Ngajilo aendelea kuwawezesha wajasiriamali Iringa

IRINGA: Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ameendelea kuonyesha dhamira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuratibu mafunzo maalumu ya ujasiriamali awamu ya pili yanayowakutanisha zaidi ya wajasiriamali 400 wa Manispaa ya Iringa.

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kuanzisha, kusimamia na kukuza biashara endelevu.

Mafunzo hayo yamekuja wakati ambapo Serikali na wadau wa maendeleo wanasisitiza umuhimu wa ujasiriamali kama nyenzo ya kupunguza umaskini, kuzalisha ajira na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa taifa.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amesema uwekezaji katika maarifa ya ujasiriamali ni hatua muhimu ya kuwawezesha vijana, wanawake na makundi mengine yenye uhitaji maalumu kujiondoa katika utegemezi wa ajira rasmi na kujenga uchumi wa kujitegemea.

Alisema katika mazingira ya sasa ambapo idadi ya wahitimu inaongezeka kila mwaka, ujasiriamali unapaswa kupewa kipaumbele kama suluhisho la changamoto ya ajira na njia ya kuongeza kipato kwa wananchi.

“Tunapowajengea uwezo wananchi kupitia mafunzo ya ujasiriamali, tunawapa nyenzo za kujikwamua kiuchumi, kuanzisha ajira kwa wengine na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla,” alisema Sitta.

Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa biashara ndogo na za kati kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, huduma za maendeleo ya biashara pamoja na fursa za manunuzi ya umma zinazoweza kutumiwa na wajasiriamali kuongeza kipato na kupanua biashara zao.

Kwa mujibu wa waandaaji, mafunzo hayo yameandaliwa kwa uratibu wa mbunge huyo kama sehemu ya mkakati wake wa kuwawezesha wananchi wa Iringa Mjini kiuchumi kupitia elimu, ubunifu na matumizi ya fursa mbalimbali za biashara.

Katibu Msaidizi wa Ofisi ya Mbunge wa Iringa Mjini, Hassan Rafiq, amesema mwitikio mkubwa wa washiriki unaonesha kuwa wananchi wengi wanatambua umuhimu wa maarifa katika mafanikio ya biashara kuliko kutegemea mtaji pekee.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea washiriki uwezo katika maeneo ya usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu, upatikanaji wa masoko, matumizi ya teknolojia na namna ya kunufaika na mifumo rasmi ya kifedha kutoka Serikali na taasisi za fedha.

“Mheshimiwa Ngajilo anaamini maendeleo ya kweli yanaanza pale wananchi wanapopata maarifa ya kujitegemea kiuchumi. Ndiyo maana ameendelea kusukuma programu hizi za mafunzo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema Rafiq.

Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha biashara zao, kuongeza tija na kutumia vyema fursa za mikopo na masoko zinazopatikana ndani na nje ya mkoa wa Iringa.

Wataalamu wa maendeleo wanaeleza kuwa ujasiriamali ni moja ya nguzo muhimu zinazotajwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani unaotegemea ubunifu, teknolojia na ushiriki mpana wa wananchi katika shughuli za uzalishaji.

Kupitia mafunzo kama hayo, vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanapata fursa ya kuingia katika uchumi rasmi, kuongeza kipato cha kaya na kushiriki kikamilifu katika safari ya kuijenga Tanzania yenye uchumi imara na jumuishi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button