Mfumo mpya wa forodha kurahisisha biashara Zanzibar

ZANZIBAR: Mfumo wa Pamoja wa Uondoshaji wa Shehena Maeneo ya Forodha Zanzibar unatarajiwa kuleta ahueni kwa wafanyabiashara kwa kurahisisha mazingira ya biashara na kupunguza urasimu uliokuwa ukiwakabili.
Kupitia mfumo huo, hatua mbalimbali za uondoshaji wa shehena zitafanyika kwa urahisi na kwa wakati, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za biashara na kuimarisha ushindani wa wafanyabiashara Zanzibar.

Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar, Saleh Haji Pandu, amesema hayo leo Juni 3, 2026 wakati akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Zanzibar.
Pandu amesema kuwa mfumo huo utaimarisha utoaji wa huduma kwa kuwezesha taasisi mbalimbali za serikali kufanya kazi kwa pamoja kupitia jukwaa moja la kidijitali.

Alifafanua kuwa kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, wafanyabiashara walilazimika kutembelea taasisi mbalimbali ili kukamilisha taratibu za uingizaji wa bidhaa na biashara, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa huduma pamoja na kuongeza gharama za uendeshaji.
Aidha, amesema kuwa uzinduzi wa mfumo huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mageuzi ya kidijitali yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa taasisi za serikali, kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi.
“Tutakapokuwa na mifumo kama hii tutapunguza kiwango cha udanganyifu, kuongeza ukusanyaji wa mapato, na serikali yetu itanufaika zaidi katika kutekeleza miradi ya maendeleo,” amesema Pandu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya TEHAMA kutoka Huduma za Forodha Korea, Kim Ki-dong, ambaye taasisi yake inasaidia katika ujenzi wa mfumo huo, alisema kuwa uboreshaji wa mifumo ya kidijitali utaimarisha utendaji wa Idara ya Forodha Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Ameongeza kuwa Taasisi ya Huduma za Forodha Korea (Korea Customs Service – KCS) itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Idara ya Forodha Tanzania katika ujenzi wa mifumo ya kisasa itakayoboresha utendaji wa forodha, hususan katika matumizi ya teknolojia za kielektroniki.
Naye Rais wa Jumuiya ya Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB), Omar Hussein Mussa, amesema kuwa kwa sasa mawakala wa forodha wanakabiliwa na changamoto ya ucheleweshaji wa uondoshaji wa mizigo kutokana na kulazimika kufika katika zaidi ya taasisi 14 ili kukamilisha taratibu zinazohitajika.
Amesema kuwa utekelezaji wa Mfumo wa Pamoja wa Uondoshaji wa Shehena Maeneo ya Forodha Zanzibar (The Zanzibar Single Window) utarahisisha mchakato huo kwa kuwawezesha mawakala na wafanyabiashara kukamilisha taratibu kwa haraka zaidi, kwa gharama nafuu na bila ya usumbufu.
“Kwa sasa tunalazimika kutembelea zaidi ya taasisi 14 na kufuatilia nyaraka mbalimbali ili kutoa shehena forodhani. Mfumo huu ukianza kufanya kazi utarahisisha shughuli hizo na kuendana na mazingira ya kisasa ya biashara duniani,” amesema Omar.
Mfumo wa Pamoja wa Uondoshaji wa Shehena Maeneo ya Forodha Zanzibar (The Zanzibar Single Window) unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kuharakisha utoaji wa huduma za biashara, kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa kodi na mapato ya serikali, pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara Zanzibar.



