Benki ya Equity zaidi kupasua anga Zanzibar

ZANZIBAR: BENKI ya Equity Tanzania imezindua rasmi kituo maalum cha huduma za kibenki cha Zanzibar Supreme katika eneo la Kijangwani, Mjini Magharibi Zanzibar, hatua inayolenga kuboresha huduma za kifedha kwa wateja wa hadhi ya juu, wawekezaji na wafanyabiashara.
Uzinduzi wa kituo hicho ulioongozwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Hamad Omar Bakar, unaifanya Benki ya Equity Tanzania kufikisha matawi mawili Zanzibar na jumla ya matawi 19 nchini kote.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank Tanzania, Isabela Maganga, Isabela Maganga amesema kufunguliwa kwa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa benki wa kuimarisha huduma za kifedha, kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kusaidia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
“Uzinduzi wa kituo cha Zanzibar Supreme ni hatua muhimu katika safari yetu ya kuendelea kusogeza huduma za kifedha karibu na wateja wetu. Kupitia kituo hiki, tunalenga kutoa huduma za kibenki zinazokidhi mahitaji ya wateja binafsi, wafanyabiashara wa kati na wakubwa, kampuni, wawekezaji na sekta ya hoteli, ambayo ni moja ya nguzo muhimu za uchumi wa Zanzibar,” amesema Maganga.
Ameeleza kuwa benki hiyo itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya huduma kwa wateja, mifumo ya kidijitali na suluhisho za kifedha zitakazowezesha ukuaji wa biashara, upatikanaji wa mitaji na uwekezaji wa muda mrefu.

Kwa mujibu wa benki hiyo, kituo cha Zanzibar Supreme kimeundwa mahsusi kuwahudumia wateja wa hadhi ya juu, wajasiriamali, kampuni, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kwa kuwapatia huduma za kibenki za kiwango cha juu zinazozingatia mahitaji yao binafsi na ya biashara.
Huduma zitakazotolewa katika kituo hicho ni pamoja na ufunguzi wa akaunti, mikopo, huduma za biashara, huduma za fedha za kimataifa, huduma za kidijitali, ushauri wa kifedha na huduma maalum kwa wateja wanaohitaji usimamizi wa karibu wa masuala yao ya kifedha.
Uzinduzi huo umeelezwa kuwa unaendana na jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kukuza uchumi shindani, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kuimarisha upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha kwa wananchi na wawekezaji.
Kwa sasa, Benki ya Equity Tanzania ina matawi 19 nchini, yakiwemo yaliyopo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma, Moshi, Mbeya, Morogoro, Geita, Kahama na Zanzibar, hatua inayodhihirisha dhamira ya taasisi hiyo ya kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi na wadau wa maendeleo ya uchumi.




