Wakulima Kagera wajiunga biashara ya kaboni

KAGERA: WAKULIMA wadogo wapatao 180,000 katika Mkoa wa Kagera tayari wamesajiliwa kushiriki katika biashara ya kaboni, hatua inayotajwa kuwa fursa mpya ya kuongeza kipato kwa wananchi huku ikichochea juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mafanikio hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa KADERES, Leonard Kachebonao, wakati wa kikao cha wadau wa biashara ya kaboni kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, kikiongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Richard Muyungi.
Kachebonao alisema kuwa licha ya kampuni hiyo kuwa changa, imefanikiwa kusajili wakulima wadogo 180,000 katika Mkoa wa Kagera, huku hatua ya usajili ikiendelea katika wilaya mbalimbali za mkoa huo kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.

“KADERES imeendelea kufanya kazi kwa karibu na jamii ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika miradi ya kaboni. Hadi sasa tumefanikiwa kusajili wakulima 180,000 na bado tunaendelea na zoezi hilo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera,” alisema Kachebonao.
Alifafanua kuwa shughuli za kampuni hiyo zinafanyika katika karibu wilaya zote za Mkoa wa Kagera isipokuwa Manispaa ya Bukoba, huku maandalizi ya kuanza utekelezaji wa shughuli hizo yakikamilishwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Dk Muyungi alisema maendeleo na ukuaji wa biashara ya kaboni nchini yanapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazochochea ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa wananchi katika kipindi cha miongo ijayo.
Alisema Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha biashara ya kaboni inasimamiwa kwa ufanisi ili iweze kutoa manufaa ya kiuchumi kwa wananchi huku ikiendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, alibainisha kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili, hususan misitu, ambayo inaweza kutumika kuzalisha mikopo ya kaboni (carbon credits) na hivyo kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Serikali inaendelea kuweka mazingira bora yatakayowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika biashara ya kaboni ili waweze kunufaika na fursa zinazotokana na sekta hii. Tunahitaji kuhakikisha kuwa ukuaji wa sekta hii unaendana na malengo ya maendeleo ya taifa na matarajio yaliyowekwa katika Dira ya 2050,” alisema Dk Muyungi.
Katibu Mkuu huyo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kuhakikisha biashara ya kaboni inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii zinazoshiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.
Mbali na Mkoa wa Kagera, KADERES imejipanga kupanua shughuli zake katika mikoa ya Morogoro na Pwani ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika miradi ya uhifadhi wa mazingira inayozalisha mikopo ya kaboni.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali na wadau mbalimbali za kuendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika biashara ya kaboni, ambayo imeendelea kupata umuhimu mkubwa duniani kama moja ya suluhisho la kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.




I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills. This is what I do….. https://www.work27.info