Trilioni 76 za maendeleo zilivyoibadili Tanzania
Mwaka 2021, mkazi wa Sumbawanga aliyekuwa akihitaji huduma ya CT Scan au matibabu ya kibingwa mara nyingi alilazimika kusafiri kilomita 326 kwenda Mbeya au zaidi ya kilomita 1,100 hadi Dar es Salaam.
Kule Kibondo mkoani Kigoma, baadhi ya wanafunzi walitembea hadi kilomita sita kufika shuleni. Kitele, Mtwara Vijijini, mvua ziliponyesha daraja lililokuwepo lilifunikwa na maji na kukata mawasiliano kati ya vijiji, shule, vituo vya afya na masoko.
Nenda pale Kishapu, Shinyanga, baadhi ya vikundi vya uzalishaji vilikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa umeme wa uhakika. Miaka mitano baadaye, simulizi hizo zinaanza kubadilika.
Nyuma ya mabadiliko hayo kuna jambo moja ambalo mara nyingi wananchi hawalioni moja kwa moja; bajeti ya Serikali.
Kati ya mwaka wa fedha 2021/22 na 2025/26, Serikali ilipitisha bajeti zenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 228. Kati ya fedha hizo, Sh trilioni 76.32 zilielekezwa moja kwa moja kwenye matumizi ya maendeleo.
Mwaka 2021/22, Serikali ilitenga Sh trilioni 13.33 kwa maendeleo. Kiasi hicho kiliongezeka hadi Sh trilioni 15 mwaka 2022/23 na kufikia Sh trilioni 15.74 mwaka 2023/24. Mwaka 2024/25 fedha za maendeleo zilikuwa Sh trilioni 14.76 kabla ya kuongezeka hadi Sh trilioni 17.49 mwaka 2025/26.
Katika kipindi hicho, bajeti kuu ya Serikali iliongezeka kutoka Sh trilioni 36.33 hadi Sh trilioni 56.49, sawa na ongezeko la asilimia 55.5 ndani ya miaka mitano.
Lakini baada ya trilioni hizo kupitishwa na kutumika, swali linabaki: Je, fedha hizo zimezalisha matokeo yanayolingana na ukubwa wa uwekezaji huo?
Mapato ya Ndani na Uwezo wa Kugharamia Maendeleo
Ukuaji wa bajeti ulienda sambamba na ongezeko la mapato ya ndani.
Takwimu za Serikali zinaonyesha mapato ya ndani yaliongezeka kutoka Sh trilioni 20.59 mwaka 2020/21 hadi Sh trilioni 29.83 mwaka 2023/24, ongezeko la zaidi ya Sh trilioni 9 ndani ya miaka mitatu.
Kwa wachumi, hiki ni kiashiria muhimu cha uwezo wa nchi kugharamia maendeleo yake yenyewe.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Lupa Ramadhani, anasema mafanikio mengi yanayoonekana leo yanahusishwa na dhamira ya kisiasa ya uongozi wa juu wa nchi.
“Political will ya Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake imewezesha mapinduzi haya ambayo jamii inayaona leo. Miradi mingi imepata msukumo wa kisiasa, fedha na usimamizi wa karibu.”
Kwa mujibu wa Dk. Lupa, ongezeko la bajeti pekee halitoshi. Kinachopaswa kupimwa ni uwezo wa fedha hizo kugeuka kuwa huduma na matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Sh Trilioni 76 Zilinunua Nini?
Mojawapo ya changamoto kubwa katika mjadala wa fedha za umma ni kwamba wananchi husikia trilioni zikitajwa lakini huwa hawaoni moja kwa moja maana yake.
Kwa lugha rahisi, trilioni 76 za maendeleo zilijigeuza kuwa hospitali, vituo vya afya, shule, reli, barabara, madaraja, minara ya mawasiliano, miradi ya maji na umeme.
Katika sekta ya afya, idadi ya vituo vya kutolea huduma imeongezeka kutoka 10,153 hadi 13,683 katika kipindi cha miaka mitano.
Hospitali zimeongezeka kutoka 404 hadi 475 huku vituo vya afya vikiongezeka kutoka 956 hadi 1,359. Idadi ya vitanda vya wagonjwa imeongezeka kutoka 86,131 hadi 153,683 na vitanda vya wagonjwa mahututi (ICU) kutoka 258 hadi 1,362.

Matokeo ya takwimu hizo yanaonekana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa iliyopo Sumbawanga.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Ismail Hosea Macha, anasema hospitali hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1974 haikuwa na uwezo wa kutoa huduma nyingi za kisasa kama ilivyo sasa.
Leo kuna CT Scan, X-Ray, Ultrasound, mtambo wa kuzalisha hewa tiba, wodi za wagonjwa mahututi na huduma mbalimbali za kibingwa ambazo hapo awali zilihitaji wagonjwa kwenda Mbeya au Muhimbili.
Mama Mwanaidi Izii, ambaye ni mmoja wa wanufaika wa huduma hizo, anasema mabadiliko hayo yamewanufaisha zaidi wananchi wa kipato cha chini.
“Tunashukuru kwa sababu huduma nyingi sasa tunazipata hapa hapa. Hata vifo vya watoto na akina mama vimepungua.”
Kwa mtazamo wa uchumi, uwekezaji katika afya hupunguza gharama za matibabu, muda wa kupoteza katika safari za kutafuta huduma na kuongeza tija ya nguvu kazi ya Taifa.
Elimu Kama Uwekezaji wa Uchumi wa Baadaye
Katika miaka ya karibuni, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya elimu.
Mwaka 2021 pekee ulishuhudia ujenzi wa madarasa 5,224, maabara za sayansi 902, mabweni 223 na maelfu ya matundu ya vyoo kupitia programu mbalimbali za maendeleo.

Wilayani Kibondo, mkoani Kigoma, zaidi ya Sh milioni 594 zilitumika kujenga shule mpya mbili za msingi za Nyabwai na Karundo.
Jackson Juma, mkazi wa Kisogwe, anasema kabla ya shule hizo kujengwa baadhi ya watoto walitembea hadi kilomita sita kila siku kufuata elimu.
“Watoto walikuwa wanachoka njiani. Sasa shule imekaribia na tunaamini hata ufaulu utaongezeka.”
Kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi, elimu ni uwekezaji wa muda mrefu unaolenga kuongeza ubora wa mtaji wa binadamu, ambao ndiyo msingi wa uzalishaji, uvumbuzi na ushindani wa Taifa.
Miundombinu na Gharama za Biashara
Kwa miaka mingi, gharama za usafirishaji zimekuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa vya ukuaji wa biashara nchini.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeongeza bajeti ya TARURA kutoka Sh bilioni 275 hadi zaidi ya Sh bilioni 772.

Fedha hizo zimewezesha ujenzi wa kilomita 1,442 za barabara za lami, kilomita 19,879 za changarawe na utekelezaji wa miradi ya madaraja 3,195 nchini. Katika Kitele, Wilaya ya Mtwara Vijijini, daraja jipya limebadili maisha ya wananchi.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Hatibu Nunu, anasema daraja hilo limeondoa changamoto za wanafunzi kushindwa kufika shule, wananchi kushindwa kupata huduma za afya na wakulima kushindwa kufikisha mazao yao sokoni wakati wa mvua.
Malori yaliyokuwa yanakwama sasa yanaweza kufika kuchukua korosho, ufuta na mazao mengine bila usumbufu.
Mabadiliko hayo yanaonekana pia katika reli ya kisasa ya SGR. Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, zaidi ya abiria milioni 2.51 walitumia reli hiyo huku zaidi ya tani 102,452 za mizigo zikisafirishwa.
Kwa lugha ya uchumi, miundombinu hiyo inapunguza gharama za biashara, kuongeza kasi ya usafirishaji na kuboresha ushindani wa uzalishaji wa ndani.
Umeme, TEHAMA na Uchumi wa Kisasa
Ukuaji wa uchumi wa kisasa unategemea zaidi nishati na mawasiliano.
Katika kipindi hicho, uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini umefikia megawati 4,522.54.
Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu umeongeza megawati 50 kwenye Gridi ya Taifa huku awamu nyingine ya megawati 100 ikitarajiwa kuanza.

Kwa Zacharia Pimbi wa Kishapu, takwimu hizo zina maana ya ajira na uzalishaji.
Anasema umeme wa uhakika umewezesha kikundi chao cha uchakataji wa ngozi kuongeza uzalishaji na kuwapatia vijana fursa za kipato.
Kwa upande wake, Lelina Emanuel Nyahigi anasema umeme umeongeza uwezo wa wanawake kushiriki shughuli za uzalishaji na biashara.
Wakati huo huo, Serikali imeendelea kuwekeza katika mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Zaidi ya kilomita 13,820 za mkongo zimejengwa huku wilaya 120 kati ya 139 zikiunganishwa na huduma hiyo.
Pia minara 758 imejengwa katika kata 713 ili kupanua upatikanaji wa mawasiliano. Kwa wachumi, miundombinu hii ndiyo msingi wa uchumi wa kidijitali unaotegemewa kuchochea biashara, ubunifu na ajira katika miaka ijayo.
Kutoka Maendeleo Hadi Uwekezaji
Mafanikio ya miaka mitano iliyopita hayaonekani kwenye miundombinu pekee.
Ripoti ya Taifa ya Uwekezaji inaonyesha Tanzania imeendelea kufanya mageuzi ya sera na sheria ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje. Hatua hizo zimejumuisha Sheria mpya ya Uwekezaji ya mwaka 2022 pamoja na kuanzishwa kwa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji mwaka 2023.
Lengo ni kuhakikisha uwekezaji wa Serikali katika miundombinu unaambatana na ukuaji wa uwekezaji wa sekta binafsi. Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, anaona mwelekeo huo kupitia msisitizo wa kuongeza thamani ya malighafi zinazozalishwa nchini.
Anasema kuchakata malighafi ndani ya nchi badala ya kuziuza ghafi kunaweza kuongeza ajira, mapato na ushindani wa viwanda vya Tanzania.
Kwa upande wake, Mbunge wa Lupembe, Edwin Swalle, anasema bajeti za miaka ya karibuni zimeonyesha dhamira ya kushughulikia changamoto za wananchi katika sekta za miundombinu, ajira, kilimo na huduma za kijamii.
Je Tanzania Inaweza Kujitegemea Zaidi?
Pamoja na mafanikio hayo, wataalamu wanaona changamoto inayofuata ni kuhakikisha maendeleo hayo yanajitegemea kifedha.
Mtaalamu wa uchumi, Dk. Hilderbrand Shayo, anasema mabadiliko yanayotokea kwa washirika wa maendeleo duniani yanaonyesha umuhimu wa Tanzania kuongeza uwezo wake wa ndani wa kugharamia maendeleo.
“Mataifa ya Ulaya nayo yanapitia changamoto zao. Haiwezi kuwa suluhisho la kudumu kuendelea kutegemea misaada yao. Tunahitaji kuimarisha uwezo wa ndani wa kuzalisha mapato na kugharamia maendeleo yetu.”
Anasema taasisi za umma zikisimamiwa vizuri zinaweza kuzalisha mapato makubwa, kuchakata rasilimali za ndani na kuongeza mchango wake katika mfuko wa Serikali.
Aidha, anasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuongeza uwekezaji, ajira na mapato.
Tafiti za ESRF zinaonyesha kuwa Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma za kijamii licha ya changamoto za COVID-19, vita vya Ukraine na misukosuko ya uchumi wa dunia. Kwa upande wake, REPOA inaeleza kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha uwekezaji wa maendeleo unaendelea kuongeza ushindani wa uchumi, kuchochea sekta binafsi na kuongeza tija ya uzalishaji.

Je Sh Trilioni 76 Zimeleta Matokeo?
Jibu la swali hilo haliwezi kupatikana kwenye jedwali la bajeti pekee. Linaonekana kwa mama ambaye hahitaji tena kusafiri mamia ya kilomita kutafuta huduma za kibingwa. Linaonekana kwa mwanafunzi ambaye hatembei tena kilomita sita kwenda shule.
Linaonekana kwa mkulima ambaye mazao yake yanafika sokoni hata wakati wa mvua. Na linaonekana kwa mjasiriamali ambaye sasa anaendesha mashine zake kwa umeme wa uhakika. Baada ya miaka mitano ya uwekezaji wa zaidi ya Sh trilioni 76 katika maendeleo, ushahidi unaonesha kuwa fedha hizo zimeanza kuonekana katika maisha ya wananchi.
Hata hivyo, kipimo kikubwa zaidi cha mafanikio ya awamu inayofuata hakitakuwa idadi ya miradi itakayojengwa, bali uwezo wa miradi hiyo kuzalisha ajira, kuongeza tija, kuvutia uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa uchumi wenye ushindani mkubwa zaidi katika Afrika.



