TPSC, IPA zatakiwa kukuza uadilifu kwa watumishi

DAR ES SALAAM: SERIKALI imetoa maagizo matano kwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) ikiwemo kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma, kufanya tafiti tumizi na kutoa ushauri wa kitaalam ili kuwaongezea uadilifu na uwajibikaji mahali pa kazi katika kufikia malengo ya Dira za Maendeleo ya Taifa 2050.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete alitoa maagizo hayo leo Dar es Salaam alipomwakilisha Makamu wa Rais,Balozi Emmanuel Nchimbi kwenye Kongamano la Pili la Utumishi wa Umma Tanzania 2026.
Alisema wanapaswa kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yalenge katika kujenga Utumishi wa Umma wenye sifa stahiki, uadilifu, uzalendo wa kitaifa, moyo wa kujituma, weledi, uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi ya Taifa.
“Mnapaswa kutoa na kusimamia kikamilifu mafunzo ya lazima katika utumishi, ikiwemo mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wa umma wapya, na kuhakikisha yanawafikia watumishi wengi zaidi katika ngazi zote za utumishi wa umma na mafunzo ya umahiri kwa kada mbalimbali ambayo yamewekwa kisheria,”alisema Kikwete.
Aliagiza kuimarishwa kwa matumizi ya matokeo ya tafiti tumizi, na shauri za kitaalamu zitakazosaidia serikali za pande zote mbili za muungano kutatua changamoto mbalimbali za kiutumishi ikiwemo kuchangia kuboresha sera, mipango na miongozo mbalimbali ya serikali.
Alisema vyuo hivyo vinapaswa kushirikiana na Wizara mama kubuni mifumo itakayowezesha watumishi wa umma kujenga utamaduni wa kujiendeleza kimaarifa ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na kiutendaji kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa Dira za Taifa 2050 kwa pande zote.
“Hakikisheni kuwa watumishi wapya wanahudhuria mafunzo ya awali katika utumishi wa umma na pengine wathibitishwe kazini baada ya kuhudhuria mafunzo elekezi ya awali,”aliagiza.
Kikwete aliziagiza Wizara zinazohusika na usimamizi wa utumishi wa umma kuhakikisha idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi na Mashirika ya Umma nchini wanatumia kikamilifu huduma zinazotolewa na vyuo hivyo ili kujenga utumishi wa umma wenye weledi katika kufikia malengo ya dira za taifa 2050.
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dk Ernest Mabonesho alitoa lengo kuu la kongamano hilo ni kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kuimarisha utendaji wa kazi katika taasisi zetu za umma katika mazingira hasa yanayobadilika kwa kasi.
Alieleza kuwa katika utekelezaji wa dira hizo,utumishi wa umma ndio nguzo imara katika kuhakikisha uchumi wa nchi yoyote unaendelea hivyo lazima sekta ya umma isiwe legelege.
Mkuu wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) Dk Shaaban Suleiman alisema uchumi imara unategemea kasi ya sayansi na teknolojia hivyo kongamano hilo linatoa fursa kwa watumishi na taasisi za umma kupata uwelewa wa namna ya kuendana na kasi ya dira za taifa 2050 hasa katika matumizi ya sayansi na teknolojia kwenye utoaji wahuduma kwa wanachi.
Naye Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya TPSC,Profesa Masoud Muruke alisema bodi hiyo inaendelea kuzihimiza taasisi zote za umma nchini kuimarisha utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii na ufanisi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.



