Kihongosi afunguka mbinu za ushindi CCM

IRINGA: Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amebainisha misingi mikuu inayokifanya chama hicho kuendelea kuaminiwa na kushinda chaguzi kuu za kiserikali nchini Tanzania.
Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Iringa, Kihongosi amesisitiza kuwa siri ya mafanikio ya CCM inajikita katika mambo makuu matatu ambayo ni utekelezaji wa Ilani, mtandao mpana wa wanachama, na weledi katika kuomba kura.
Kihongosi ameeleza kuwa CCM inashinda kwa sababu ina Ilani ya uchaguzi inayotekelezeka kwa vitendo, ikijikita katika kutatua kero za msingi za wananchi kama upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi ikiwemo maji, umeme, barabara, kilimo, elimu na afya.
Alitolea mfano wa miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Julius Nyerere, na miradi ya umwagiliaji kama ule wa Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo kama kielelezo cha ahadi zinazotekelezwa.

Aidha, alisisitiza kuwa amani na utulivu ndio msingi mkuu unaowezesha maendeleo hayo kuonekana kote nchini.
Akifafanua sababu ya pili, Kihongosi amesema tofauti na vyama vingine, CCM ni chama chenye watu na mtandao mpana hadi ngazi ya mashina.
Katika kuthibitisha mtandao huo, amekagua uhai wa chama katika mashina mbalimbali na kuridhishwa na uimara wa mabalozi na viongozi wa ngazi za chini.
Amesema kuwa nguvu ya chama hicho inatokana na kuwa na wanachama wengi na wakereketwa ambao wako tayari kukilinda na kukisemea chama chao wakati wote, jambo ambalo washindani wao wameshindwa kulifikia.
Amesema siri ya tatu ya ushindi ni utaalamu wa chama katika kuomba ridhaa ya wananchi kwa kutumia rekodi ya utekelezaji wa ahadi.
Kihongosi ameeleza kuwa CCM haitegemei maneno tupu, bali inaomba kura kwa kuonyesha matunda ya kazi iliyofanyika katika sekta za afya, elimu, na miundombinu.
Aliongeza kuwa chama kiko tayari kwa mijadala na hoja, akiwaalika hata wapinzani kujadiliana kuhusu ujenzi wa nchi badala ya kuibomoa.
Katika hatua nyingine, Kihongosi ametoa onyo kali kwa watumishi wa umma wanaozorota katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema kuwa CCM ina wajibu wa kuisimamia serikali ili kuhakikisha fedha za walipakodi zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Kuna watumishi wa umma wanasema chama kinawafuatafuata; waambieni tutawafuata kweli kweli kama hamtekelezi wajibu wenu,” alisisitiza Kihongosi.



