Mapato madini yaongezeka

MOROGORO: WIZARA ya Madini imesema mapato ya fedha yatokanayo na makusanyo ya madini yamevuka lengo la makadirio yaliyowekwa ya Sh trilioni 1.2 na kufikia Sh trilioni 1.36 katika kipindi cha Januari 2025 hadi Juni 23, 2026 ikiwa sawa na asilimia 113.34.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Yahaya Samamba amesema hayo Juni 24, 2026 Mjini Morogoro kwenye kikao kazi kilichoishirikisha Menejimenti ya Tume ya Madini, Wakaguzi Wasaidizi wa Madini pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara ikiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Mhandisi Samamba amesema asilimia 40 ya makusanyo hayo yanatokana na mchango wa wachimbaji wadogo pamoja na ushirikiano kati ya wizara, Tume ya Madini na wadau wengine wa sekta hiyo.
Mbali na makusanyo hayo yaliyovuka lengo, Katibu Mkuu amesema Serikali inayo mikakati mbalimbali ikiwemo inayofanyiwa kazi ya kudhibiti utoroshaji wa madini pamoja na kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo nchini.

“Mimi nikiwa msimamizi wa watumishi wa wizara ya madini nimeona nikutane na taasisi zenye wajibu wa kukusanya mapato ambayo ni Tume ya Madini, tumeweza kufanya tathimini ya wapi tumefanya vizuri na mapungufu yetu ni yapi na nini tunatakiwa tuboreshe katika mwaka wa fedha wa 2026/2027,”amesema Mhandisi Samamba.
Katibu Mkuu amesema kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 Serikali imeiwekea Wizara ya Madini lengo la kukusanya kiasi cha Sh trilioni 1.4.

Mbali na hayo pia amesema limepitishwa pendekezo la Bunge linaliitaka asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na madini yabaki ndani ya wizara hiyo kwa ajii ya kuendeleza shughuli za utafiti mkubwa wa madini.
Mhandisi Samamba amesema hadi sasa kwenye utafiti mkubwa umeshafanywa kwa asilimia 16 hata hivyo,Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameagiza wizara ufanyike utafiti zaidi ya asilimia hizo.

“Sisi tunaamini nchi itakapofanyiwa utafiti zaidi na kufikia asilimia 100 basi mapato yanayotokana na madini yanaweza kuwa maradufu na yanaweza kusaidia bajeti yetu kuu ya Serikali,”amesema Mhandisi Samamba.
Kwa upande wake wa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk Janet Lekashigo amesema tume hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwenye usimamizi na udhibiti wa sekta ya madini kwa weledi na uwajibikaji mkubwa.
Mwenyekiti wa Tume hiyo amesema kikao hicho kinawapa nafasi muhimu ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa majukumu yao ya mwaka wa fedha 2025/2026 na kujadili mafanikio na changamoto zilizotokea na kuweka mkakati madhubuti wa kuanza mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ari mpya ya mwelekeo imara.
Dk Lekashigo ameihakikishia wizara kwamba tume hiyo itaendelea kutekeleza kwa wakati maagizo, maelekezo na miongozo itakayotolewa na wizara kwa lengo la kuimarisha sekta ya madini.
Awali, Kamishna wa Tume ya Madini, Dk Abdulhaman Mwanga ameeleza umuhimu wa sekta ya madini na ushirikiano wa taasisi nyingine zilizopo chini ya wizara kwa kuunda utatu kwenye shughuli za sekta ya madini nchini.
Dk Mwanga amezitaja taasisi hizo ni STAMICO pamoja na Taassisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).



