Madini yanavyochangia maendeleo ya elimu, maendeleo ya jamii

TARIME: KIASI cha Sh bilioni 9.4 zimeelekezwa kuboresha shule, makazi ya walimu na kuwawezesha watoto kupata mazingira bora ya kujifunzia
Katika vilima vya Tarime ambako dhahabu imekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa eneo hilo, hazina nyingine yenye thamani kubwa zaidi inaendelea kung’ara.
Hazina hiyo si dhahabu inayochimbwa ardhini, bali ni uwekezaji katika elimu ya watoto ambao unajenga msingi wa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.
Wakati Bara la Afrika linaadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika mwezi Juni kila mwaka kwa kutafakari haki, ustawi na mustakabali wa watoto, Kampuni ya Barrick kupitia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara imeendelea kuonesha namna sekta ya madini inavyoweza kuwa chachu ya maendeleo ya jamii kwa kuwekeza katika elimu.
Tangu mwaka 2019, Barrick imewekeza jumla ya Sh bilioni 26.9 katika miradi 255 ya maendeleo ya jamii inayotekelezwa katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
Kati ya fedha hizo, asilimia 35 sawa na Sh bilioni 9.4 zimeelekezwa kwenye sekta ya elimu.
Uwekezaji huo umeleta mabadiliko makubwa katika maeneo ambayo kwa miaka mingi yalikuwa yakikabiliwa na changamoto za miundombinu duni ya shule, utoro wa wanafunzi, viwango vya juu vya kuacha shule na mazingira magumu ya kujifunzia, hususan kwa watoto wa kike.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru, Juma Kengoe, amesema mafanikio makubwa ya mgodi huo hayawezi kupimwa kwa kiasi cha dhahabu kinachochimbwa pekee, bali kwa mchango wake katika kujenga maisha bora ya vizazi vijavyo.
“Kipimo halisi cha mafanikio yetu si dhahabu inayochimbwa, bali mustakabali tunaoujenga kwa watoto hawa ambao ndiyo tegemeo la taifa,” amesema.
Kwa mwaka 2025 pekee, Barrick ilikamilisha miradi 25 katika shule za msingi na miradi mingine 26 katika shule za sekondari zinazozunguka mgodi huo.
Miradi hiyo ilihusisha ujenzi wa madarasa ya kisasa yaliyopunguza msongamano wa wanafunzi pamoja na kuondoa matumizi ya miundombinu chakavu.
Aidha, ujenzi wa mabweni mawili kwa ajili ya wanafunzi wa kike unaendelea, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya masomo na kuongeza fursa za watoto wa kike kuendelea na elimu.
Miradi hiyo pia imehusisha ujenzi wa nyumba za walimu ili kuwahakikishia mazingira bora ya kuishi na kufanya kazi, sambamba na upatikanaji wa madawati, meza na viti vya walimu, vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na miundombinu ya maji.

Mwalimu John Mwita, ambaye amefundisha katika Wilaya ya Tarime kwa zaidi ya miaka 15, amesema maboresho hayo yameleta tofauti kubwa katika utoaji wa elimu.
“Kulikuwa na nyakati ambazo tulifundisha chini ya miti. Mvua iliponyesha masomo yalikatika. Leo tuna madarasa bora, baadhi yakiwa na umeme. Hali hii imeongeza ari ya wanafunzi na walimu,” amesema.
Mbali na uwekezaji katika miundombinu, Barrick imeendelea kuwawezesha wanafunzi kupitia Mpango wa Friends of North Mara unaotekelezwa katika shule 10 za sekondari zinazozunguka mgodi huo.
Kupitia programu hiyo, wanafunzi hupata mafunzo mbalimbali ya kuwawezesha kujenga stadi za maisha na ujuzi unaowaandaa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.

Mafunzo hayo yanajumuisha elimu ya fedha na uwekezaji, ambapo vijana hufundishwa namna ya kuweka akiba, kuanzisha miradi na kutumia fursa za kiuchumi zinazowazunguka.
Aidha, wanaelimishwa kuhusu utunzaji wa mazingira ili kujenga kizazi kinachotambua umuhimu wa kuoanisha maendeleo na uhifadhi wa mazingira.
Programu hiyo pia imekuwa jukwaa muhimu la kupinga ukeketaji, tatizo ambalo bado linaendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Tarime.
Kupitia elimu hiyo, wavulana na wasichana hujengewa uelewa kuhusu haki za binadamu, usawa wa kijinsia na umuhimu wa kulinda utu wa mtoto wa kike.
Mnufaika wa mpango huo, Neema Samweli, amesema mafunzo hayo yamepanua uelewa wake kuhusu maisha zaidi ya darasani.
“Nimegundua kuwa elimu siyo kufaulu mitihani pekee. Inatufundisha namna ya kufanya maamuzi sahihi, kujilinda na kuwa raia wenye mchango chanya katika jamii,” amesema.
Kwa upande wake, Grace Peter, mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye umri wa miaka 17 katika moja ya shule zinazoshiriki mpango huo, amesema elimu aliyopata imebadilisha mtazamo wake kuhusu maisha na mustakabali wake.
“Kabla ya kujiunga na programu hii sikuwa na uelewa kuhusu kuweka akiba wala haki zangu kama msichana. Leo nawafundisha hata dada zangu wadogo yale ninayojifunza. Ndoto yangu ni kuwa wakili ili niweze kutetea na kulinda haki za wasichana wengine,” amesema.
Uwekezaji unaofanywa na Barrick kupitia Mgodi wa North Mara unaendelea kudhihirisha kuwa maendeleo ya kweli hayaishii kwenye uchimbaji wa rasilimali za madini pekee, bali yanapatikana pale rasilimali hizo zinapotumika kujenga maarifa, uwezo na matumaini ya watoto ambao ndiyo viongozi wa kesho.



