Ushirikiano Tanzania, Sweden waimarisha elimu

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ushirikiano wa miaka 63 kati ya Tanzania na Sweden umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu,matumizi ya nishati safi, utafiti na ujenzi wa rasilimali watu nchini.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 63 ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Sweden,Profesa Mkenda alisema ushirikiano huo umewezesha ujenzi wa vyuo, mafunzo kwa walimu na kuimarisha elimu ya ujuzi kwa Watanzania.

Alisema Tanzania na Sweden zinaingia katika hatua mpya ya ushirikiano unaojengwa katika misingi ya usawa na maslahi ya pamoja, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika elimu ya juu, utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia.

Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya vyuo vikuu na taasisi za utafiti za Tanzania na Sweden unapaswa kuimarishwa zaidi ili kuendeleza tafiti zinazotoa suluhisho kwa changamnoto za maendeleo na kuandaa kizazi chenye maarifa na ujuzi wa kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.

Balozi wa Sweden nchini Tanzania,Charlotta Macias alisema Sweden haitaacha kushirikiana na Tanzania kwa sababu uhusiano baina ya nchi hizo mbili unaendelea kukuwa kwa kasi.

Alisema licha ya kushirikiana katika maeneo ya elimu,nishati jadidifu wataendelea kushirikiana katika masuala ya uwekezaji.

“Tangu tulipoanza kushirikiana na Tanzania tumefanikiwa kushirikiana katika masuala ya usambazaji wa umeme vijijini, nishati ya umeme na maji, usimamizi wa fedha za umma, ulinzi wa jamii, utafiti na elimu, pamoja na haki za binadamu na usawa wa kijinsia,”alisema Balozi Macias.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button