MIAKA 31 YA KUTAFUTA HAKI
Ndani ya migogoro ya ardhi na mirathi inayozitikisa familia za Watanzania

Chini ya kivuli cha miti mikubwa, meza ya plastiki ya buluu iligeuka kuwa ukumbi wa muda wa kusikiliza ushahidi.
Juu yake kulikuwa na kompyuta mpakato, mafaili yaliyofungwa kwa utepe, nakala za hati za ardhi na nyaraka za mahakama zilizokusanywa kwa zaidi ya miongo mitatu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisimama akiwa ameshika kipaza sauti. Pembeni yake walikuwa maafisa wa ardhi, wanasheria, polisi na wajumbe wa kamati maalumu aliyoiunda kuchunguza mgogoro wa nyumba iliyopo Kiwanja Na. 317, Regent Estate.
Mbele yake alikaa Bi Everlin Chiomba. Mikono yake ilitikisika alipokuwa akieleza simulizi ambayo, kwa mujibu wa maelezo yake, ilianza zaidi ya nusu karne iliyopita.
“Nilifunga ndoa mwaka 1968,” alieleza mbele ya kamati. “Mume wangu, Raphael Andrew Chiomba, alifariki mwezi Februari mwaka 1993.”
Baada ya kifo hicho, alisema alifungua shauri la mirathi katika Mahakama ya Mwanzo Kawe mwaka 1995 ili kusimamia mali za marehemu.

Hapo ndipo mgogoro ulipoanza.
Kwa mujibu wa maelezo yake, wakati shauri la mirathi likiendelea, watu walijitokeza wakidai kuwa nyumba hiyo ilikuwa tayari imeuzwa mwaka 1995. Akapinga madai hayo. Mahakama ikaagiza ushahidi uwasilishwe.
Kwa mujibu wa maelezo ya Bi Everlin Chiomba, Jeshi la Polisi lilifanya uchunguzi wa kitaalamu wa maandishi baada ya mahakama kutoa maelekezo hayo. Anadai matokeo ya uchunguzi huo yalionyesha kuwa saini iliyokuwa kwenye hati ya mauziano haikuwa saini halisi ya marehemu mume wake. Hata hivyo, mgogoro haukuishia hapo.
Miaka ikapita. Mashauri yakahamishwa kutoka mahakama moja kwenda nyingine.
Mahakimu wakabadilika. Majaji wakabadilika. Lakini mgogoro uliendelea kuishi. Siku hiyo ya Mei 6, 2026, haikuwa tena kesi ya kawaida ya nyumba.
Ilikuwa ni mwisho wa safari iliyokuwa imeanza kwa kifo cha Raphael Andrew Chiomba mwezi Februari 1993, ikaingia mahakamani mwaka 1995 na kuendelea kwa zaidi ya miongo mitatu.
Baada ya kusikiliza pande zote na kupitia taarifa ya kamati maalumu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alitangaza kuwa kwa mujibu wa nyaraka zilizopo na maamuzi ya Mahakama, nyumba hiyo ilikuwa inamilikiwa na Godifrey Shuma na Carista Shuma.
Bi Everlin Chiomba alielekezwa kuondoka katika nyumba hiyo, huku akielezwa kuwa endapo hangeridhika na uamuzi huo, sheria bado ilikuwa inampa haki ya kurejea mahakamani.
Kwa wengi waliokuwapo eneo hilo, ulikuwa mwisho wa mgogoro mmoja. Lakini kwa mwandishi, tukio hilo lilifungua swali kubwa zaidi.

Iwapo mgogoro mmoja wa nyumba ungeweza kuanzia mwaka 1995 na bado ukawa unazungumziwa Mei 2026, hali ikoje kwa maelfu ya Watanzania wengine wanaokabiliwa na migogoro ya ardhi na mirathi? Jibu linaanza kuonekana kwenye takwimu rasmi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Katiba na Sheria, kati ya Julai 2025 na Machi 2026, migogoro ya ardhi ndiyo ilikuwa sababu kubwa zaidi iliyowapeleka wananchi kutafuta msaada wa kisheria, ikichukua asilimia 32 ya mashauri yote yaliyopokelewa. Migogoro ya mirathi ilifuata kwa asilimia nane.
Katika kipindi hicho, wananchi 7,462,387 walifikiwa na huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni na programu mbalimbali za Serikali. Hata hivyo, nyuma ya kila asilimia kuna jina.
Kuna mjane anayepigania nyumba aliyokuwa akiishi na familia yake. Kuna watoto wanaogombea urithi wa wazazi wao. Kuna mnunuzi aliyelipa fedha zake lakini bado hajakabidhiwa mali aliyonunua.
Na kuna familia ambazo baada ya mazishi ya mzazi, safari yao mpya huanzia mahakamani. Ndipo uchunguzi huu ulipoanzia.
Tatizo Kubwa Kuliko Nyumba Moja
Simulizi ya Bi Everlin Chiomba si ya kipekee.
Miezi michache kabla ya uamuzi wa Mei 6, Dar es Salaam ilishuhudia mgogoro mwingine uliotikisa hisia za umma.
Alice Nyamwiza Haule, mjane wa marehemu Justus Rugaibula, alidai kuvamiwa nyumbani kwake na kushuhudia mali zake zikitolewa nje baada ya kuzuka mgogoro wa umiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi.
Baada ya malalamiko hayo kufikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, iliundwa kamati maalumu ya kuchunguza madai ya pande zote.
Uchunguzi wa kamati hiyo ulibaini kuwa nyumba hiyo ilikuwa mali ya ndoa na kwamba mkopo uliokuwa umechukuliwa na marehemu mume wake haukuhusisha nyumba hiyo. Serikali baadaye ilimkabidhi Alice hati ya nyumba pamoja na Sh milioni 10, huku ikisisitiza kuwa haki za wananchi zinapaswa kulindwa kwa kuzingatia ushahidi na sheria.
Wakati Bi Everlin Chiomba na Alice Haule wakipitia safari ndefu za migogoro ya nyumba, Mkoa wa Arusha ulitoa taswira tofauti ya namna migogoro inaweza kutatuliwa bila kuongeza mlundikano wa kesi mahakamani.
Adela Molel, mkazi wa Muriet jijini Arusha, aliongoza familia yake kufuatilia mgogoro wa ardhi uliotokana na mirathi ya marehemu Nathani Molel. Kwa mujibu wa wahusika, pamoja na kuwapo kwa uamuzi wa mirathi uliotolewa mwaka 2015 chini ya usimamizi wa Juliana, msimamizi wa mirathi, mgawanyo wa mali uliendelea kuzua malalamiko kati ya warithi na baadhi ya wanunuzi wa ardhi.
Walalamikaji walisema walizunguka katika ofisi mbalimbali za serikali wakitafuta suluhu, lakini mgogoro uliendelea kuathiri mahusiano ya familia na matumizi ya ardhi.
Hatimaye, suala hilo lilifikishwa katika timu yaKampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Haki tumeiona, na tumeridhika
Afisa Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, George Onyango Daniel, anasema timu hiyo ilianza kwa kuwasikiliza walalamikaji kabla ya kuwaita upande mwingine kwenye meza ya mazungumzo.
“Kulikuwa na shida, ilibidi tushauri, na walituelewa kwa kuwa pande zote walikubali kumaliza tatizo,” alisema.
Baada ya mazungumzo hayo, pande zote zilikubaliana kutekeleza makubaliano waliyoyafikia badala ya kuanzisha mgogoro mwingine mahakamani.
“Haki tumeiona, na tumeridhika,” alisema Adela Molel baada ya kufikiwa kwa makubaliano, akieleza kuwa kilichowasaidia zaidi hakikuwa kushinda kesi, bali kupata suluhu iliyorudisha amani ndani ya familia.
Visa hivi vitatu—Mikocheni, Kariakoo na Arusha—vinaonyesha sura tofauti za tatizo moja.
Migogoro mingi ya ardhi na mirathi haianzi mahakamani. Huanzia ndani ya familia. Huanzia kwenye urithi ambao haukuandikwa.
Huanzia kwenye mikataba isiyoeleweka. Huanzia kwenye mauzo yanayopingwa. Na mara nyingi huishia kutumia miaka mingi katika ofisi mbalimbali za Serikali na Mahakama. Tatizo hilo linaonekana wazi kwenye takwimu rasmi.
Chanzo: Wizara ya Katiba na Sheria, Julai 2025–Machi 2026.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera anasema migogoro ya ardhi iliongoza kwa kuchukua asilimia 32 ya mashauri yote yaliyowasilishwa kupitia huduma za msaada wa kisheria. Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, pia anakiri kuwa migogoro ya ardhi imeendelea kutawala malalamiko ya wananchi, katika ziara zake kote nchini akizitaka taasisi zinazohusika kuongeza uwajibikaji na kuharakisha utatuzi wa migogoro hiyo.
“Takribani robo tatu ya hoja zote nilizopokea zinahusu migogoro ya ardhi,” Alisema Waziri Mkuu Aprili 19, 2026 wakati akiwa katika ziara yake mkoani Dodoma kusikiliza kero za wananchi. “Hii imenishangaza … kwani watendaji na baadhi ya maafisa wa ardhi wanafanya kazi gani?”
Ukweli ni kwamba wakati jitihada za msaada wa kisheria na usuluhishi zikiendelea, takwimu za Mahakama ya Tanzania zinaonesha kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Mahakama zilikuwa na jumla ya mashauri 205,038.
Mashauri mapya 159,851 yalifunguliwa na 166,553 yakahitimishwa. Hata hivyo, mashauri 38,485 yaliendelea kusubiri usikilizwaji, huku 3,675 yakiwa ni mashauri ya muda mrefu.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mfumo wa utoaji haki unaendelea kushughulikia idadi kubwa ya migogoro kila mwaka, huku migogoro ya ardhi na mirathi ikiendelea kuwa sehemu kubwa ya changamoto zinazowakabili wananchi.
Lakini pamoja na takwimu hizo, viongozi wa sekta ya sheria wanaamini kuwa si kila mgogoro unapaswa kuishia mahakamani.
Haki Kupitia Mazungumzo
Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji George Mcheche Masaju, amekuwa akisisitiza matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), akisema zimeonesha uwezo wa kuokoa muda, kupunguza gharama na kudumisha amani kati ya pande zinazohusika. Amesema changamoto kubwa iliyobaki ni kwamba wananchi wengi bado hawazifahamu ipasavyo, hivyo wadau wa sheria wanapaswa kuongeza elimu kuhusu matumizi yake.
Mtazamo huo unaonekana katika simulizi ya Adela Molel wa Muriet, Arusha. Baada ya mgogoro wa mirathi ulioendelea licha ya kuwapo kwa uamuzi wa mwaka 2015, pande zilizokuwa zikivutana zilikubali kuketi pamoja mbele ya timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC). Badala ya kuanzisha kesi nyingine, walikubaliana kutekeleza suluhu waliyoifikia.
Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria na Mratibu wa Kampeni MSLAC, Ester Msambazi, anasema kampeni hiyo ilianzishwa kusogeza huduma za sheria karibu na wananchi, hasa wasioweza kuzifikia kutokana na gharama, umbali au ukosefu wa elimu ya kisheria.
“Mbali na ushauri wa kisheria, kampeni hii hutoa elimu, huandaa nyaraka za kisheria na kusaidia kusuluhisha migogoro kabla haijafika mahakamani,” anasema.
Msambazi anaeleza kuwa uzoefu wa kampeni unaonyesha migogoro mingi inayoripotiwa inahusu ardhi, mirathi, ndoa na kazi. Anasema Serikali imepeleka mawakili na wataalamu wa sheria nchini kote ili kuwasaidia wananchi kupata haki kwa wakati, huku akibainisha kuwa migogoro mingi ya ardhi hutokana na migawanyiko ya urithi, kutokuandika wosia na migogoro ya kifamilia.
Kwa Adela, ushindi haukuwa kumshinda mtu mahakamani. “Haki tumeiona, na tumeridhika,” alisema baada ya makubaliano kufikiwa. Lakini simulizi ya Bi Everlin Chiomba inaonyesha upande mwingine wa mfumo huo.
Mei 6, 2026, baada ya kusikilizwa kwa zaidi ya saa kadhaa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bi Everlin aliondoka Regent Estate bila nyumba aliyokuwa ameitetea kwa zaidi ya miongo mitatu. Hata hivyo, hakunyimwa haki ya kuendelea kutafuta haki kupitia Mahakama kama hataafiki uamuzi uliotolewa.
Safari ya Bi Everlin Chiomba ilianza mwaka 1995. Ya Adela Molel iliishia kwenye meza ya usuluhishi. Katikati ya simulizi hizo mbili ndipo inapopimwa taswira halisi ya mfumo wa haki nchini Tanzania—si kwa misingi ya sheria pekee, bali kwa maisha ya wananchi unaoyagusa kila siku.



