CHAKULA, DIPLOMASIA NA USHAWISHI

Jinsi Tanzania inavyojijenga kuwa mhimili wa usalama wa chakula EAC

Asubuhi ya Mei 16, 2026, shughuli za usafirishaji wa mazao katika mpaka wa Holili unaounganisha Tanzania na Taveta nchini Kenya zilisimama kwa muda.

Haikuwa kwa sababu ya ukame. Wala haikuwa kwa sababu ya mavuno kupungua mashambani.

Kilichosimama ulikuwa ni mtiririko wa biashara.

Ndani ya saa chache tu, athari zikaanza kuonekana upande wa Kenya. Migahawa ilianza kukosa baadhi ya bidhaa, wauzaji wa mboga wakaanza kutafuta mazao kwa gharama kubwa zaidi, huku bei ya viazi ikipanda kutoka shilingi 250 hadi 400 kwa kilo.

“Tunachukua bidhaa nyingi za chakula kutoka Holili, na mimi husafirisha chakula pekee si abiria. Ninaona jinsi mama lishe na migahawa wanavyopata shida kwa sababu walitegemea usafirishaji wangu,” anasema Abdi Suleiman, mfanyabiashara anayesafirisha mazao kati ya Holili na Taveta.

Tukio hilo lilidumu kwa muda mfupi, lakini lilifunua ukweli mkubwa ambao kwa muda mrefu haukuwa ukitazamwa kwa uzito.

Leo hii, Tanzania si taifa linalozalisha chakula kwa ajili ya wananchi wake pekee.

Tanzania, imekuwa mhimili muhimu wa mfumo wa usambazaji wa chakula unaounganisha Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Malawi na Msumbiji. Mtiririko wa mazao kutoka Tanzania unapokatizwa, athari zake huanza kuonekana haraka katika masoko ya nchi jirani.

Katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kimataifa na kupanda kwa gharama za uzalishaji wa chakula, uwezo wa taifa kuzalisha chakula umeanza kuwa zaidi ya mafanikio ya kilimo.

Umekuwa nyenzo ya ushawishi wa kiuchumi na diplomasia ya kikanda.

Lakini Tanzania imefikaje hapa?

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, mwaka 2025 Tanzania ilizalisha zaidi ya tani milioni 23.78 za mazao ya chakula, kiwango kilichowezesha taifa kufikia zaidi ya asilimia 130 ya kujitosheleza kwa chakula. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa nchi inazalisha chakula kinachozidi mahitaji ya wananchi wake, hatua inayoiwezesha kushiriki katika biashara ya kikanda na kutoa msaada wa chakula wakati wa dharura.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa uzalishaji mkubwa pekee hautoshi kuifanya Tanzania kuwa mhimili wa usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), changamoto ya dunia si kuongeza uzalishaji pekee, bali kuhakikisha chakula kinazalishwa kwa njia endelevu, kinahifadhiwa vizuri na kinawafikia walaji hata wakati wa majanga.

Kevin Gichangi, Meneja wa Mpango wa Rift Lakes wa WWF-Kenya, anasema changamoto za sasa zinahitaji suluhisho linalounganisha uzalishaji wa chakula na uhifadhi wa mazingira.

“Mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bioanuwai, uharibifu wa ardhi na ukosefu wa chakula vinahitaji suluhisho jumuishi linalounga mkono watu na mazingira kwa wakati mmoja,” anasema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa kilimo ikolojia kutoka Biovision Foundation, Eliane Steiner, anasema usalama wa chakula wa baadaye utategemea uwezo wa nchi kujenga mifumo ya uzalishaji inayoongeza mavuno bila kuharibu mazingira.

“Mifumo ya kilimo ikolojia huongeza ustahimilivu, huimarisha usalama wa chakula, lishe na kipato cha wakulima huku ikihifadhi bioanuwai na huduma muhimu za mazingira,” anasema.

Kauli hizo zinaonyesha kuwa katika karne ya sasa, yenye ushindani wa mataifa, (usalama wa chakula) hautapimwa kwa ukubwa wa ardhi ya kilimo pekee, bali kwa uwezo wa kuhakikisha chakula kinapatikana wakati wote na kinaweza kuwafikia hata majirani wakati wa dharura.

Tanzania imeanza kuonyesha uwezo huo.

Mwezi Machi 2026, Serikali ya Tanzania ilitoa msaada wa tani 500 za mahindi kwa Serikali ya Msumbiji kufuatia mafuriko makubwa yaliyoathiri uzalishaji wa chakula nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, alisema hatua hiyo ilikuwa ishara ya uhusiano wa karibu uliodumu kwa miongo mingi kati ya mataifa hayo mawili.

“Rais Samia amenituma kufikisha msaada huu ili uweze kuwapunguzia adha waathirika wa mafuriko, na Tanzania ipo tayari kuendelea kutoa msaada kwa Msumbiji katika nyakati zote,” alisema.

Kwa mtazamo wa kawaida, huo ulikuwa msaada wa kibinadamu. Lakini kwa mtazamo wa diplomasia ya kisasa, ulikuwa ujumbe mpana zaidi. Ulionyesha kuwa Tanzania inatumia uwezo wake wa kuzalisha chakula kama nyenzo ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuchangia uthabiti wa usalama wa chakula kwa Afrika Mashariki na Kusini.

PIA SOMA: Diplomasia ya Tanzania ilivyofungua fursa za uchumi miaka 5 ya Samia

Wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia na uchumi wanakiri kuwa uwezo huo haukujengwa kwa bahati.

Ni matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu katika uzalishaji wa kilimo, umwagiliaji, hifadhi ya chakula, miundombinu ya biashara na sera zinazolenga kuifanya sekta ya kilimo iwe kichocheo cha maendeleo ya uchumi.

Swali linalobaki sasa si kama Tanzania inaweza kujilisha. Swali ni jinsi ilivyoweza kujenga mfumo unaoiwezesha kuwa mshirika wa kimkakati katika usalama wa chakula wa ukanda mzima.

Majibu yake yanapatikana katika safari iliyoanza zaidi ya miongo miwili iliyopita, wakati Tanzania ilipoanza kuunganisha kilimo, biashara na diplomasia katika mkakati mmoja wa maendeleo—mkakati ambao leo unaanza kuifanya nchi ionekane kwa jicho tofauti ndani ya Afrika Mashariki na Kusini.

Mfumo unaobadili nafasi ya Tanzania

Safari ya Tanzania kuwa mhimili wa usalama wa chakula haikuanza na msaada wa tani 500 za mahindi kwenda Msumbiji. Msingi wake ulianza kujengwa zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Mwaka 2004, viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walikutana jijini Arusha kuzindua Mpango wa Kimkakati wa Maendeleo wa Kikanda (RISDP), ulioweka usalama wa chakula kuwa moja ya nguzo kuu za maendeleo ya ukanda.

Akizindua mpango huo akiwa Mwenyekiti wa SADC, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, alisema baada ya vita vya ukombozi wa kisiasa, Afrika ilikuwa inaanza vita mpya.

“Leo tunapigana vita tofauti; vita dhidi ya umaskini na kunyimwa fursa za maendeleo.”

Miaka zaidi ya ishirini baadaye, dira hiyo inaendelea kutafsiriwa kwa vitendo. Mwezi Mei 2026, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Kilimo wa SADC uliofanyika Victoria Falls nchini Zimbabwe, ambapo viongozi walijadili mikakati ya pamoja ya kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha biashara ya mazao na kujenga mifumo ya kilimo inayostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Lakini kuwa mhimili wa usalama wa chakula hakumaanishi kuzalisha mazao mengi pekee. Kunahitaji mfumo unaounganisha uzalishaji, masoko, hifadhi na usafirishaji.

Ndiyo maana Serikali imeendelea kuimarisha Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), ambayo mwaka 2026 ilitangaza mpango wa kununua hadi tani milioni 1.2 za nafaka. Hatua hiyo imelenga kuongeza akiba ya taifa, kutoa soko la uhakika kwa wakulima na kuimarisha uwezo wa Tanzania kukabiliana na mahitaji ya ndani na ya kikanda wakati wa dharura.

Wakati huohuo, Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya masoko. Mwezi Mei 2026, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, alizindua Soko la Mazao la Kibakwe wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma, kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha biashara ya mazao nchini.

“Rais Dk. Samia ni mtendaji ambaye akisema jambo, anatekeleza. Haya yanadhihirishwa na kazi kubwa iliyofanyika,” alisema.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mhandisi Athuman Kilundumya, soko hilo ni sehemu ya Programu ya Tanzania Food Systems Resilience Program (TFSRP), inayolenga kuboresha masoko, uhifadhi na usafirishaji wa mazao. Linatarajiwa kuhudumia wakulima na wafanyabiashara zaidi ya 300 kwa wakati mmoja, kuongeza ajira na kupanua masoko ya mazao ya ukanda wa kati wa Tanzania.

Kwa Profesa Esther Kokunywanisa Ishengoma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mafanikio hayo hayawezi kuwa endelevu bila ujumuishaji wa kifedha.

“Maendeleo ya kweli hutokea pale maarifa yanapotumika mahali yanapohitajika zaidi. Ujumuishaji wa kifedha haupaswi kuwa fursa kwa wachache; unapaswa kuwa haki kwa wote,” anasema.

Kwa mtazamo wake, wakulima hawawezi kunufaika kikamilifu na soko la kikanda bila kupata mitaji, elimu ya biashara na huduma za kifedha zinazowawezesha kuongeza thamani ya mazao yao.

Katika ngazi ya uzalishaji, Tanzania imeanza pia kuwekeza katika kilimo ikolojia. Kupitia mradi wa Baridi Sokoni, zaidi ya wakulima 10,000 huko Morogoro, Njombe, Kilimanjaro na Zanzibar wameanza kutumia mbinu zinazoboresha rutuba ya udongo, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mavuno. 

Uzalishaji wa viazi umeongezeka kutoka wastani wa tani 8 hadi 10 kwa hekta na kufikia tani 12 hadi 14, huku wakulima wa viungo mkoani Morogoro wakiongeza bei ya mauzo kutoka takribani Sh13,000 hadi Sh20,000 kwa kilo kupitia masoko ya pamoja. Wanawake ni asilimia 65 ya wanufaika wa mradi huo.

Kwa Reguli Marandu wa WWF Tanzania, mafanikio hayo yanatokana na kuimarisha maarifa yaliyopo katika jamii.

“Tunachopaswa kufanya ni kuimarisha yale ambayo tayari yanafanya kazi.”

Jenipher Tairo wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine anaamini kuwa mustakabali wa usalama wa chakula utategemea uwekezaji katika sayansi ya kilimo, huduma za ugani na ubunifu unaoongeza tija bila kuharibu mazingira.

Lakini hata mazao mengi hayawezi kuleta matokeo kama hayawezi kufika sokoni kwa wakati.

Mchumi na mhadhiri wa uchumi, Dk. Blasius Kahyoza, anasema mafanikio yanayoonekana katika Bandari ya Dar es Salaam yametokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ulioanza mwaka 2016/17.

“Maboresho hayo yameongeza uwezo wa bandari kuhudumia mizigo mingi zaidi, kupunguza muda wa huduma kwa meli na kuongeza ushindani wa Tanzania kama lango muhimu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati,” anasema.

Hatua hizo zinaenda sambamba na juhudi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za kuoanisha mifumo ya ukaguzi wa mazao ili kurahisisha biashara ya kikanda. Wakati biashara ya mazao imeendelea kufungua fursa mpya za ajira katika maeneo ya mipakani kama Newala na Holili, ambapo vijana na wafanyabiashara wananufaika na ongezeko la usafirishaji wa mazao kwenda nchi jirani.

Hata hivyo, changamoto bado zipo. Mabadiliko ya tabianchi, ushindani wa masoko na hitaji la kuongeza thamani ya mazao vinaendelea kuhitaji uwekezaji zaidi katika umwagiliaji, maghala, teknolojia, usindikaji na huduma za kifedha kwa wakulima.

Pamoja na changamoto hizo, ushahidi unaonyesha kuwa Tanzania imeanza kujenga mfumo unaounganisha uzalishaji wa chakula, hifadhi, masoko, miundombinu na diplomasia katika mkakati mmoja wa maendeleo.

PIA SOMA: Jinsi diplomasia ya uchumi ilivyoifanya Tanzania kuwa kitovu kipya cha uwekezaji wa madini Afrika 

Asubuhi ile ya Mei 16, 2026, lori ziliposimama Holili, wengi waliona ni changamoto ya kawaida ya mpakani.

Lakini ndani ya saa chache, migahawa Taveta ilianza kukosa bidhaa, wafanyabiashara wakaanza kutafuta mboga kwa bei ya juu zaidi, na bei ya viazi ikapanda kutoka shilingi 250 hadi 400 kwa kilo.

Kilichosimama hakikuwa lori pekee. Ulikuwa mtiririko wa chakula uliounganisha uchumi wa nchi mbili. Tukio hilo lilifunua ukweli ambao takwimu za uzalishaji haziwezi kuueleza peke yake.

Tanzania imefikia hatua ambayo mazao yake yanapoacha kusafiri, athari zake huanza kuonekana katika masoko ya nchi jirani.

Hapo ndipo maana halisi ya diplomasia ya chakula inaanza kujitokeza. Karne iliyopita, mataifa mengi yalijenga ushawishi kupitia madini, mafuta na nguvu za kijeshi. Leo, katika dunia inayokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kimataifa na ongezeko la mahitaji ya chakula, ushawishi unaweza pia kujengwa kupitia uwezo wa kuzalisha, kuhifadhi na kusambaza chakula.

Kwa ushahidi wa takwimu, sera, uwekezaji na nafasi yake ndani ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania inaanza kujenga ushawishi huo. Huenda hiyo ndiyo sababu dunia inaanza kuiangalia Tanzania kwa jicho tofauti. Si kwa sababu ina ardhi kubwa ya kilimo. Bali kwa sababu imeanza kuwa sehemu ya jibu la swali ambalo mataifa mengi yanauliza leo: Tutawalishaje watu wetu kesho?

Tanzania imeanza kuthibitisha kuwa chakula si zao la kilimo pekee. Ni nyenzo ya uchumi. Ni nyenzo ya ushirikiano. Na katika karne ya 21, kinaweza kuwa moja ya zana muhimu zaidi za diplomasia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button