Wagonjwa 1200 kutibiwa macho

ZAIDI ya wagonjwa 1,200, sawa na asilimia 25 ya wagonjwa wanaofika katika Kliniki za Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, wanatarajiwa kunufaika na vipimo na matibabu ya kibingwa ya macho, baada ya Taasisi ya Vision Care kutoa mashine ya kisasa ya kupima macho yenye thamani ya Sh milioni 50.8.

Akizungumza wakati wa kupokea mashine hiyo, Mkuu wa Idara ya Upasuaji, Dk. Godlove Mfuko, amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, Taasisi ya Vision Care pamoja na Shirika la Kimataifa linalojihusisha na kuzuia upofu duniani kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA), wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano kuanzia 2026 hadi 2030 lengo likiwa ni kuimarisha huduma za matibabu ya macho nchini.

“Mashine hii ni kama ultrasound ya jicho, lakini inatumia teknolojia ya mwanga badala ya mawimbi ya sauti. Ina uwezo wa kuchunguza jicho lote kwa sekunde tano na kutoa taarifa muhimu, hususan kuhusu sehemu ya nyuma ya jicho,” amesema Dk. Mfuko.

Ameongezea kuwa kifaa hicho kina uwezo wa kugundua mapema magonjwa ya macho kama vile presha ya macho (glaucoma) na matatizo ya retina, hivyo kurahisisha matibabu ya haraka kabla ya hali kuwa mbaya na kusababisha upofu. SOMA: Wagonjwa 823 kufanyiwa upasuaji macho

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, Dk. Julieth Magandi, ameishukuru Vision Care kwa kuendelea kushirikiana na hospitali hiyo tangu mwaka 2020, akibainisha kuwa ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya ya macho nchini.

“Leo tumefanya upya makubaliano yetu ya ushirikiano kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Hii inaonesha dhamira ya pamoja ya kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi kupitia ushirikiano wenye tija,” alisema Dk. Magandi.

Ameeleza kuwa kabla ya msaada huo, hospitali hiyo haikuwa na mashine ya OCT, na ujio wake sasa utaongeza uwezo wa kufanya uchunguzi wa kina wa magonjwa ya macho kwa haraka zaidi, na kutoa majibu ndani ya muda mfupi, hatua itakayoboresha ubora wa huduma kwa wagonjwa.

Nae, Mkurugenzi wa Vision Care Tanzania, Jienun Park amesema ushirikiano huo ulianza mwaka 2017, na kupitia ufadhili wa KOICA wameendelea kuimarisha huduma za macho nchini Tanzania. Amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa vifaa tiba, dawa, pamoja na mafunzo kwa wataalamu wa afya ili kuwajengea uwezo zaidi katika kipindi chote cha utekelezaji wa makubaliano hayo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button