Apewa ubalozi wa utalii Tanzania

DAR ES SALAAM: Mfanyabiashara na mtangazaji wa utalii, Khalid Hamed Al Barwani,, ameikabidhi Serikali gari la kihistoria aina ya Jeep Wrangler alilotumia katika safari kutoka Oman hadi Tanzania kama zawadi kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, huku akiteuliwa kuwa Balozi wa Hiari wa Utalii Tanzania kutokana na mchango wake katika kuitangaza Tanzania kimataifa.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Khalid amesema uamuzi wa kulikabidhi gari hilo unatokana na kutambua mchango mkubwa wa Rais Samia katika kuimarisha na kuitangaza sekta ya utalii, akieleza kuwa ameongoza juhudi za kuitangaza Tanzania duniani na kuongeza mafanikio ya sekta hiyo.

Amesema gari hilo lina historia ya kipekee kwa kuwa lilitumiwa katika safari iliyopita nchi zaidi ya 10 kabla ya kuwasili Tanzania na baadaye kutembelea karibu asilimia 90 ya vivutio vya utalii nchini, jambo linalolifanya kuwa sehemu ya historia ya utangazaji wa utalii wa Tanzania.

Khalid ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kuunga mkono safari hiyo tangu ilipoanzishwa, akisema ushirikiano huo umechangia kufanikisha lengo la kuitangaza Tanzania katika soko la kimataifa.

Aidha, ameahidi kutumia nafasi yake kama Balozi wa Hiari wa Utalii kuitangaza Tanzania kwa nguvu zaidi katika nchi za Ghuba kupitia lugha ya Kiarabu, Kiswahili na Kiingereza, huku akisisitiza umuhimu wa Watanzania wenyewe kutembelea na kuthamini vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Amesema kupitia timu yake ya Dream Team Explorers wataendelea kutumia mbinu bunifu za kutangaza utalii kwa kufanya safari za kutumia magari ya aina ya 4×4 yenye namba za usajili kutoka nchi za Kiarabu, hatua inayovutia wananchi wa mataifa hayo kufuatilia vivutio vya Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, aliyemwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema uteuzi wa Khalid Baruan umetokana na mchango wake mkubwa katika kutangaza utalii wa Tanzania kupitia safari yake iliyopita zaidi ya nchi 10 na kutembelea karibu asilimia 90 ya vivutio vya utalii nchini.

Mafuru amesema wizara itaendelea kuwatambua na kuwateua mabalozi wa hiari miongoni mwa wadau na watu binafsi wanaotoa mchango mkubwa katika kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi, akibainisha kuwa Khalid ameahidi kuendelea kuwa balozi wa utalii wa Tanzania katika nchi za Ghuba.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button