TFS yapongezwa kurejesha hekta milioni 3.3 za misitu

MOROGORO: OFISI ya Makamu wa Rais imewapongeza wadau wa mazingira ukiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Mradi wa Urejeshaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai nchini kwa kufanikisha kurejesha ardhi ya misitu iliyoharibiwa hekta milioni 3.3  kufikia Desemba 2024.

Naibu Katibu Mkuu wa  Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano), Abdalah Mitawi ametoa pongezi hizo  jana mjini Morogoro alipofungua warsha ya kujenga uwezo kikosi-kazi cha taifa cha urejeshaji wa mazingira ya ardhi na misitu iliyoharibika.

Mitawi amesema katika kuchangia jitihada za kimataifa na malengo ya uhifadhi mazingira kitaifa, mwaka 2018, Serikali ya  Tanzania iliahidi kurejesha hekta milioni 5.2 za maeneo ya ardhi na misitu iliyoharibika kufikia mwaka 2030  chini ya mkakati wa  African Forest Landscape Restoration Initiative (AFR100).

Amesema, mwaka 2024 kupitia mradi huo ilikamisheni kwa taasisi ya  Kituo cha Kufuatilia Hewa ya Kaboni (NCMC) kufanya tathmini ya utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kurejesha hekta milioni 5.2 za ardhi na misitu iliyoharibiwa ikiwa na lengo la kujipima hatua tuliyofikia.

Mitawi amesema katika taarifa ya tathmini imeonesha kuwa utekelezaji wa ahadi hiyo upo kwenye hatua nzuri  ikibainisha kuwa kiasi cha hekta milioni 3.3 zilikuwa zimerejeshwa kufikia mwezi Desemba 2024.

“Nitoe wito kwa wadau wote wa mazingira kuendeleza jitihada hizi katika maeneo mbalimbali ili kufikia mwaka 2030 itakapofanyika tathmini nyingine tuwe tumevuka lengo hili “ amesema Mitawi.

Mitawi amesema pamoja na  utajiri mkubwa, Tanzania bado  inakabiliwa na changamoto za uharibifu wa mazingira, ambapo tafiti zimeonesha kuwa nchi yetu inapoteza takribani hekari 469,000 za misitu kila mwaka.

Amesemauharibifu huo unachangiwa na shughuli za kibinadamu zisizoendelevu kama vile wa idadi kubwa ya mifugo isiyolingana na uwezo wa malisho na unyweshaji wa mifugo kwenye vyanzo vya maji, ukataji wa misitu kwa ajili ya kuni na mkaa, uanzishaji wa mashamba mapya unaotokana na kilimo cha kuhamahama na uchimbaji holela wa madini.

Mitawi amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kisera na kimkakati kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa na wadau wa maendeleo zinazolenga kuongeza kasi ya kuhifadhi mazingira na urejeshaji wa ardhi ya misitu iliyoharibiwa ni sehemu ya ajenda muhimu ya maendeleo endelevu ya Tanzania.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Uzalishaji Mbegu za  Miti wa TFS , Dk Hamza Katety, kwa niaba ya Kamaishna wa Uhifadhi TFS,  ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kutokana na ushirikiano wake kupitia miradi ya Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF), ambapo  Wakala huo ni mfufaika kuitumia kwenye maendeleo ya uhifadhi wa misitu nchini.

Dk Katety amesema kuwa tangu kuanza mkakati huo wa Serikali kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa takwimu na kuwajua wadau wanaojihusisha na kazi hiyo na maeneo yao .

“Njia pekee ambayo tunafiriki inaweza kutusaidia kwa haraka  kupata takwimu ni kuwa na jukwaa la pamoja la wadau wanaotekeleza  jukumu hili,” amesema Dk Katety .

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button