Massana Mwishawa aichukua rasmi hatamu TANAPA

ARUSHA: Uongozi mpya ndani ya Shirika kongwe la uhifadhi nchini umechukua hatamu rasmi baada ya aliyekuwa Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA CPA Musa Nassoro Kuji kumaliza muda wake wa uongozi na kukabidhi kijiti hicho kwa Kamishna mpya wa Uhifadhi – TANAPA Massana Mwishawa, makabidhiano yaliyofanyika Julai 08, 2026 Makao Makuu ya Shirika hilo Majengo jijini Arusha.

Kamishna Mwishawa aliteuliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Julai 02, 2026 na jana Julai 09, 2026 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji alimvika cheo kipya na kumuapisha ili kuliongoza Shirika hilo linalosimamia Hifadhi za Taifa 21 nchini zenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 97,099 ambazo ni sawa na asilimia 10.23 ya eneo lote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya nyaraka na vitendea kazi mbalimbali, Kamishna wa Uhifadhi (Mst.) CPA. Musa Nassoro Kuji alisema;

“Natoa shukrani zangu kwa Mhe. Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kuliongoza Shirika hili,  viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Wadhamini, watumishi na wadau wote kwa ushirikiano walionipatia katika kipindi chote cha uongozi wangu kwani mafanikio yote yaliyopatikana yametokana na mshikamano, weledi na kujituma kwa pamoja.”

Aidha, Kamishna Kuji aliongeza, “Lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho, ninastaafu utumishi wa umma nikiwa na furaha ya kuona mengi tumeyafikia kwa umoja wetu, niko tayari kutoa ushauri na mchango wangu kila mtakapouhitaji kwani mafanikio ya TANAPA yataendelea kuwa fahari yangu.”

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA Massana Mwishawa alisema kuwa majukumu ya taasisi anayokabidhili leo ni dhamana kubwa, alimuhakikishia mtangulizi wake na watanzania kuwa ataifanya kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili shirika hilo lifikie adhma ya serikali ya watalii milioni nane ifikapo 2030.

Kamishna Mwishawa  aliongeza, “Kuaminiwa na kupewa jukumu hili na Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kiasi kikubwa umetokana na mchango wa mapendekezo yako, hivyo nikuahidi kuendeleza misingi ile ulioiacha ya uwazi, uwajibikaji na ubunifu katika kuiongoza TANAPA”.

Sambamba na hilo Kamishna Mwishawa aliwataka maafisa na askari wote kuendeleza utamaduni wa TANAPA wa kushirikiana, kutoa ushauri na mapendekezo panapohitajika ili kufikia malengo ya Taasisi.

Kamisha Mwishawa ni mbobezi katika nyanja za Uhifadhi, ulinzi mkakati wa maliasili na utalii na ana Shahada ya Uzamili katika Masuala ya Usimamizi wa Maliasili, kabla ya uteuzi wake Julai 02, 2026 alikuwa ni Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara nafasi aliyoitumikia kuanzia Aprili 29, 2024 baada ya kuteuliwa na Bodi ya Wadhamini – TANAPA.

Vilevile, Kamishna Mwishawa ameshika nyadhifa mbalimbali katika Shirika hilo ikiwemo Meneja wa Ulinzi – TANAPA Makao Makuu (2015 – 2019), Mkuu wa Kanda ya Mashariki, Mkuu wa Hifadhi za Taifa Serengeti na Kisiwa cha Rubondo, pia alihudumu kama Mkuu wa Kitengo cha Himasheria – Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button