Serikali yataka wanahabari kuhamasisha nishati safi ya kupikia

MOROGORO — Serikali imevitaka vyombo vya habari kutumia nafasi yao kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kusaidia kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema waandishi wa habari wana nafasi muhimu ya kujenga mtazamo wa jamii na kuhamasisha mabadiliko ya tabia kupitia habari, makala na vipindi vinavyoelimisha wananchi.

Amesema kwa sasa asilimia 28 ya Watanzania ndiyo wanatumia nishati safi ya kupikia, chini ya lengo lililowekwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034.

“Waandishi wa habari wanawafikia wananchi moja kwa moja. Wakibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia, ujumbe huo utawafikia Watanzania wengi zaidi,” Salome alisema wakati akifungua warsha ya wanahabari kuhusu kampeni ya nishati safi ya kupikia inayoendelea mkoani Morogoro.

Makamba amesema taarifa sahihi zinaweza kubadili mtazamo wa jamii, huku taarifa potofu zikihatarisha juhudi za serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kulinda mazingira.

Aliongeza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanachangia uhifadhi wa mazingira, afya ya wananchi, ajira kwa vijana, usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.

Meneja wa Mradi kutoka Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuendeleza Mitaji (UNCDF), Imanuel Muro, alisema mradi wa miaka minne uliofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kwa euro milioni 19.4 umesaidia kuongeza uelewa na kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Alisema wananchi wanahitaji taarifa zinazozingatia mazingira ya maeneo yao kwa kuwa teknolojia, gharama na uwezo wa watumiaji hutofautiana kutoka eneo moja hadi jingine.

“Tunahitaji kampeni za elimu zitakazoondoa hofu kuhusu nishati safi. Watu wengi bado wanaamini kupikia kwa umeme ni gharama kubwa kuliko LPG, jambo ambalo si sahihi katika mazingira yote,” alisema.

Mkurugenzi wa Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia katika Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, alisema wizara imewakutanisha wanahabari, maafisa habari wa serikali na wadau ili kuhakikisha ujumbe unaotolewa kwa umma unakuwa sahihi na unaoendana na mkakati wa mawasiliano wa taifa.

Alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia yanajumuisha gesi ya kupikia (LPG), umeme, gesi asilia (CNG), ethanoli na nishati ya jua.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills.
    This is what I do…..    https://www.work27.info

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button