Marekani yawabana raia wake wanaotoka DRC

MAREKANI imewataka raia wake wanaoondoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kukaa nje ya nchi hiyo kwa siku 21 kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini. Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia tahadhari ya Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) iliyosema wasafiri wanaotoka DRC, Uganda na Sudan Kusini watafuatiliwa afya zao kwa siku 21.
Kwa mujibu wa CDC, baadhi ya wasafiri wanaweza kuzuiwa kupanda ndege kuelekea Marekani hadi watakapomaliza kipindi hicho cha ufuatiliaji, huku watakaoruhusiwa kuingia wakifanyiwa uchunguzi wa afya katika viwanja vya ndege. SOMA: Serikali yahimiza tahadhari ya Ebola, yasema Tanzania ni salama
Ubalozi wa Marekani umeonya kuwa raia wake waliopo DRC wanapaswa kutarajia kuchelewa kwa safari na huenda wakalazimika kupitia nchi nyingine kabla ya kurejea Marekani. Wakati huo huo, mamlaka za afya nchini DRC zimesema mlipuko wa Ebola unaendelea kuenea katika maeneo mapya.
Hadi Julai 13, wagonjwa 2,011 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo na watu 754 walifariki dunia katika majimbo matano, huku Ituri ikiongoza kwa maambukizi mapya. Kwa mujibu wa mamlaka za afya nchini humo zimesema kiwango cha vifo kimefikia asilimia 37.5, kikionyesha ukubwa wa athari za virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo.



