Teknolojia za TARI zavutia wakulima Nanenane Iringa

IRINGA: Wakulima waliojitokeza katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kwa mara ya kwanza mkoani Iringa wameendelea kuvutiwa na teknolojia bunifu zinazowasilishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), huku taasisi hiyo ikisisitiza kuwa matumizi ya matokeo ya tafiti ndiyo njia ya kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na kipato cha wakulima.

Katika banda la TARI Kituo cha Kifulilo, wakulima wamekuwa wakipata elimu ya moja kwa moja kuhusu mbegu bora, miche ya matunda, teknolojia za kudhibiti magonjwa na wadudu, pamoja na mbinu za kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyapeleka sokoni.

Mratibu wa Kitengo cha Uhamishaji wa Teknolojia na Ushirikiano wa TARI Kifulilo, Lilian Ngusi, alisema ushiriki wa taasisi hiyo katika maonesho hayo unalenga kuunganisha matokeo ya tafiti na mahitaji halisi ya wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija zaidi na kupata masoko yenye ushindani.

Alisema TARI ina vituo 20 vya utafiti nchini, huku Mkoa wa Iringa ukiwa na Kituo cha Kifulilo pamoja na vituo vidogo vya Satondale, Ipogolo na Isimani vinavyoendelea kutoa huduma za utafiti na ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.

Ngusi alisema miongoni mwa teknolojia zilizovutia wageni ni mbegu bora za viazi mviringo, viazi lishe, maharage, soya na miche bora ya parachichi, pamoja na bidhaa mbalimbali zilizoongezwa thamani ili kuonesha namna mazao yanavyoweza kuleta faida kubwa zaidi kuliko kuuzwa yakiwa ghafi.

Alifafanua kuwa kwa zao la viazi mviringo, TARI inawahimiza wakulima kuingia kwenye uchakataji kwa kuzalisha bidhaa kama chipsi, hatua inayoweza kuongeza thamani ya mazao na mapato ya kaya.

Kwa upande wa viazi lishe, alisema tafiti za taasisi hiyo zimewezesha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo mikate na tambi, ambazo zimeongeza matumizi ya zao hilo pamoja na fursa za biashara.

Aidha, alisema TARI imeendelea kuboresha mbegu za maharage na soya zenye tija kubwa, huku soya aina ya Uyole ikitajwa kuwa na kiwango kikubwa cha protini kinachofaa kutengeneza vyakula vya lishe kama uji, hususan kwa watoto na makundi yenye mahitaji maalumu ya lishe.

Kwa wakulima wa matunda, Ngusi alisema taasisi hiyo inazalisha miche bora ya parachichi na kutoa mafunzo ya kitaalamu kuhusu uzalishaji, utunzaji wa mashamba na mbinu za kudhibiti wadudu na magonjwa ili kuongeza mavuno yenye ubora wa soko.

Pia TARI imewasilisha teknolojia za mitego maalumu ya kunasa wadudu waharibifu wa matunda pamoja na ubunifu mwingine unaosaidia kupunguza hasara baada ya mavuno na kuongeza tija katika uzalishaji.

Ngusi alisema dhamira ya TARI ni kuhakikisha teknolojia zote zinazotokana na tafiti hazibaki maabara, bali zinawafikia wakulima moja kwa moja na kuchangia kuongeza usalama wa chakula, kuinua kipato cha wananchi na kuifanya sekta ya kilimo kuwa yenye tija na ushindani zaidi.

“Utafiti una thamani pale unapobadilisha maisha ya mkulima. Ndiyo sababu tumekuja Nanenane kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwaonesha teknolojia zinazoweza kuongeza uzalishaji na kipato,” alisema Ngusi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button