Kampuni ya SBL yashinda tuzo kimataifa

DAR ES SALAAM; Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imeendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya bidhaa zake tatu kushinda Tuzo za Gold Quality Awards 2026 zinazotolewa na taasisi ya kimataifa ya Monde Selection yenye makao yake Brussels, Ubelgiji.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Ugavi wa SBL, Joseph Cheloti, amesema ushindi huo ni uthibitisho wa dhamira ya kampuni ya kuendelea kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa, huku ikiwekeza katika teknolojia, mifumo madhubuti ya uzalishaji na matumizi ya malighafi bora.
Cheloti alisema tuzo hizo pia ni chachu kwa kampuni kuendelea kuboresha ubora wa bidhaa zake na kuwapatia watumiaji nchini Tanzania na katika masoko ya kimataifa vinywaji vinavyokidhi matarajio yao.
“Bidhaa zilizotunukiwa tuzo hizo ni Serengeti Lite, Serengeti Lager na Serengeti Lemon, hatua inayothibitisha ubora wa bidhaa za kampuni katika soko la kimataifa.
“Tuzo za Monde Selection hutolewa kwa bidhaa zinazofikia viwango vya juu vya ubora baada ya kufanyiwa tathmini ya kina inayohusisha wataalamu wa kimataifa katika vigezo mbalimbali ikiwemo ladha, ubora wa malighafi, usalama wa bidhaa na kuridhika kwa mtumiaji.
“Mafanikio hayo yanaongeza hadhi ya Serengeti Breweries Limited kama moja ya wazalishaji wakubwa wa vinywaji barani Afrika, huku yakionesha uwezo wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania kushindana na kushinda katika jukwaa la kimataifa la ubora.” amesema.



