Mfumo wa usajili waboreshwa Brela

DODOMA:WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umebainisha kuwa umefanya maboresho makubwa katika mfumo wake wa usajili ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika maonesho ya wakulima nane nane jijini Dodoma, Ofisa Usajili wa BRELA, Yusuf Mwasakafyuke, amesema wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali, ikiwemo usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa leseni za biashara Kundi A pamoja na huduma zinazohusiana na usajili wa alama za biashara na viwanda.

Amesema uwepo wa BRELA katika maonesho hayo unalenga pia kuwahamasisha wakulima wanaofanya kilimo cha kibiashara kurasimisha shughuli zao ili waweze kujiamini zaidi katika kufanya biashara na kufikia masoko na wadau mbalimbali.

“Tunawahamasisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanaofanya shughuli mbalimbali za kilimo kufika hapa na kupata huduma ambazo wangeweza kuzitafuta wakiwa ofisini, lakini sasa wanaweza kuzipata hapa,” amesema Mwasakafika.

Vilevile, amesema BRELA inatumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu mfumo mpya wa usajili ulioboreshwa, ambao umefanyiwa maboresho ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza changamoto ambazo baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakikumbana nazo.

Kwa mujibu wa Mwasakafyuke, kupitia mfumo huo mpya, baadhi ya huduma zinaweza kufanyika kwa njia ya mtandao bila mhusika kulazimika kufika moja kwa moja katika ofisi za BRELA.

Amesema miongoni mwa maboresho yaliyofanyika ni kuwezesha uwasilishaji wa nyaraka mbalimbali kwa njia ya mfumo, ikiwemo nyaraka zinazohusiana na madeni yanayohitaji kuwasilishwa katika usajili.

“Kwa kutumia mfumo huu, sasa tumeweza kuboresha huduma kiasi kwamba mtu anaweza kuwasilisha nyaraka akiwa nyumbani kwake au benki, bila kulazimika kufika BRELA,” amesema.

Hata hivyo, amewasisitiza wananchi wanaotaka kutumia mfumo huo kuhakikisha wanakuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), namba ya simu inayotumika pamoja na anuani sahihi ya barua pepe, ambazo ni muhimu katika kupata huduma kupitia mfumo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button