Mwenge wazindua madarasa Kagongwa

SHINYANGA: Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi la jengo la vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Sekondari Kagongwa iliyopo Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Ujenzi wa jengo hilo ulianza kwa nguvu za wananchi waliotoa mchango wa shilingi milioni saba, huku ukamilishaji wake ukifadhiliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kupitia mapato ya ndani kwa kiasi cha Sh milioni 63.

Mwang’onda alisema hayo leo baada ya Mwenge wa Uhuru kupokelewa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kagongwa ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, alipokea mwenge huo.
Amesema amefurahishwa na hatua ya wananchi kushirikishwa katika ujenzi huo na amekubali kuweka jiwe la msingi kwa kuwa mradi huo umefikia hatua nzuri ya ukamilishaji. Aidha, aliwataka wazazi kusimamia maendeleo ya watoto wao na kuhakikisha wanapata elimu bora ili waweze kufaulu katika masomo yao.
Mwang’onda pia aliikabidhi shule hiyo cheti kwa ajili ya Klabu ya Wapinga Rushwa yenye wanafunzi 60, iliyoanzishwa mwaka 2023. Amesema klabu hiyo inaendelea kutoa elimu na kushiriki katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, jambo ambalo ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama.

“Nimezindua pia upandaji wa miti katika shule hiyo. Mazingira yanapaswa kutunzwa na kusimamiwa vizuri, na kila mwanafunzi anatakiwa awe na mti wake wa kuutunza. Hii itasaidia kuboresha mazingira ya kujisomea,” amesema Mwang’onda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema mwenge huo utakimbizwa katika halmashauri tatu za Ushetu, Msalala na Kahama.
Amesema mwenge huo utapita kwenye miradi 21 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 5.4 na utakimbizwa umbali wa kilomita 361.4.



