Luizer ampongeza Asha Baraka

MSANII wa muziki wa dansi nchini, Luizer Nyoni Mbutu amempongeza Asha Baraka kwa mchango wake katika kuendeleza muziki wa dansi, akisema kupitia Bendi ya Twanga Pepeta imeweza kutoa ajira kwa zaidi ya familia 40.
Luizer amesema Asha ni mwanamke mwenye juhudi na asiyekata tamaa, akimtaja kama mmoja wa watu walioendelea kupigania maendeleo ya bendi hiyo na muziki wa dansi kwa ujumla. “Ni mwanamke na nusu, ni mpambanaji asiyekata tamaa. Leo hii ni Mbunge wa Viti Maalumu, amepambana kwa miaka mingi hadi kupata nafasi hiyo, lakini pia ameipigania Bendi ya Twanga Pepeta kwa muda mrefu,” amesema Luizer.
Amesema mchango wa Twanga Pepeta hauishii katika burudani pekee bali pia umekuwa chanzo cha ajira kwa wasanii na wafanyakazi mbalimbali, hivyo kusaidia familia nyingi kupata kipato. Kwa mujibu wa Luizer amesema juhudi alizofanya Asha Baraka ni mfano wa namna sanaa inavyoweza kuchangia katika uchumi na kuwasaidia watu kujipatia kipato kupitia vipaji na ajira zinazotokana na sekta hiyo. SOMA: Bella, El Saadat, Twanga Pepeta kukiwasha Valentine Day



