Mbegu bora, chachu ya kilimo cha ushindani

IRINGA: Wakulima mkoani Iringa wametakiwa kuanza maandalizi ya msimu mwingine wa kilimo kwa kuchagua na kutumia mbegu bora, zilizoidhinishwa na zenye uwezo wa kuongeza uzalishaji, huku wakisisitizwa kuachana na mbegu zinazoweza kuathiri mavuno na kipato.
Wito huo umetolewa katika kijiji cha Mawala, kata ya Ilole katika halmashauri ya wilaya ya Kilolo, wakati wakulima wakijiandaa kwa msimu mwingine wa kilimo na kupewa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya mbegu bora katika kuongeza tija na ubora wa mazao.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mgongolwa Agrovet and Seeds, ambayo ni wakala mkuu wa mbegu zinazozalishwa na Taasisi ya Mbegu Tanzania (ASA) kwa Mkoa wa Iringa na Nyanda za Juu Kusini, Joseph Mgongolwa, amesema maandalizi mazuri ya msimu yanapaswa kuanzia kwenye uchaguzi wa mbegu, kwa kuwa ubora wa mbegu una nafasi kubwa katika kuamua kiwango na ubora wa mavuno.

Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora zenye ruzuku kwa bei nafuu, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kuwasaidia wakulima kupunguza gharama za uzalishaji.
“Wakati huu ambao wakulima wanaelekea kuanza maandalizi ya msimu mwingine, ni muhimu wasisubiri mpaka muda wa kupanda ufike. Wanapaswa mapema kupanga aina ya zao watakalolima, kutafuta mbegu bora na kushauriana na wataalamu ili kuhakikisha wanakwenda shambani wakiwa wamejiandaa,” amesema Mgongolwa.
Amesema ASA huzalisha mbegu za mazao mbalimbali, ikiwemo mahindi, maharage, alizeti na ufuta, ambazo zinaweza kuwasaidia wakulima kuongeza tija na kuzalisha mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Amesema matumizi ya mbegu bora yanapaswa kwenda sambamba na kuzingatia kanuni nyingine za kilimo, ikiwemo muda sahihi wa kupanda, nafasi za kupanda, matumizi sahihi ya mbolea, udhibiti wa magonjwa na wadudu pamoja na usimamizi mzuri wa shamba.

“Lengo si kupata mavuno mengi pekee, bali kupata mazao yenye ubora unaokubalika katika masoko. Tunataka mkulima aweze kuzalisha kwa ajili ya chakula, lakini pia awe na uwezo wa kuuza na kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mawala, Vedasto Mbuta, amewataka wakulima kutumia mbegu zinazotambulika na kuthibitishwa na Wizara ya Kilimo na kuhakikisha wanazinunua kutoka kwa wauzaji wanaoaminika.
Amesema baadhi ya wakulima wamekuwa wakikumbwa na hasara kutokana na kununua mbegu zisizojulikana, jambo linaloweza kusababisha mbegu kutoota vizuri, mavuno kuwa madogo au mazao kutofikia ubora unaotarajiwa.
“Tunapokwenda kwenye msimu mwingine, mkulima anatakiwa kujiandaa mapema. Asiangalie bei ya mbegu pekee, aangalie ubora na chanzo chake. Mbegu bora ni uwekezaji unaoweza kumrudishia mkulima faida kubwa wakati wa mavuno,” amesema Mbuta.
Baadhi ya wakulima walioshiriki katika zoezi hilo wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kutambua umuhimu wa kuanza maandalizi ya msimu mapema, hususan katika kuchagua mbegu sahihi na kupata ushauri wa wataalamu.
Wamesema wamejifunza kuwa kuongeza uzalishaji hakutegemei ukubwa wa eneo la shamba pekee, bali pia ubora wa mbegu, matumizi ya teknolojia sahihi na kufuata kanuni bora za kilimo.
Mwisho.



