Serikali yaongeza bil 20/- upanuzi JNIA

DAR ES SALAAM: SERIKALI imetoa Sh bilioni 20 kwa ajili ya kuendelea na malipo ya fidia kwa wananchi wa eneo la Kipunguni wanaopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambapo jumla ya Sh bilioni 86 kati ya Sh bilioni 114 zinazohitajika ikiwa tayari imelipwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombakaleo, amesema fedha hizo ni sehemu ya mwendelezo wa awamu za malipo na kwamba zoezi hilo litaendelea kadiri fedha zitakavyopatikana, ambapo mpaka sasa wafidiwa 717 wamelipwa, huku wananchi wengine 1,147 wakisubiri malipo yao.

Akitoa taarifa hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari, Mombakaleo amesema leo Septemba 22, 2026 TAA imepokea Sh bilioni 20 na kwamba malipo ya awamu hiyo yataanza Jumatatu, huku utaratibu wa malipo ukitolewa na Mkurugenzi wa Fedha wa mamlaka hiyo.

“Naomba niwahakikishie tumepokea Sh bilioni 20 na Jumatatu tutaanza kulipa. Maelekezo ya utaratibu wa kulipwa Mkurugenzi wa Fedha atatoa ili kila mmoja aweze kujua utaratibu na ajue kama yupo kwenye zamu ya awamu hii au awamu ijayo,”

“Naomba nichukue nafasi hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Kipunguni na wananchi wengine ambao wameamua kuvumilia kwa kuwa zoezi linaendelea na tutalipa kwa awamu. Kila mmoja atalipwa,” amesema Mombakaleo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa TAA, Mohamed Seif, amesema Sh bilioni 20 zilizotolewa zitalipwa kwa wananchi waliokamilisha kujaza fomu na kufuata taratibu zilizowekwa.

Seif amewataka wananchi wanaosubiri fidia kuendelea kuwa wavumilivu, huku akisema kuwa mamlaka inaendelea na taratibu za kuhakikisha malipo yanafanyika ndani ya muda mfupi.

Amesema wananchi waliopo kwenye orodha ya malipo ya awamu hiyo watapatiwa fomu kupitia wenyeviti wa mitaa na Serikali za mitaa na baada ya kujaza fomu hizo, walengwa watazipeleka benki kwa ajili ya uhakiki na kisha kuzirudisha TAA kwa hatua zinazofuata.

Zoezi hilo ni sehemu ya mpango wa upanuzi wa eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), unaohitaji wananchi waliopo kwenye maeneo yanayohusika kuondoka baada ya kukamilishiwa taratibu za fidia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button