TADB yaimarika, yadhamiria kuwafikia wakulima wadogo

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuimarisha shughuli zake na kuongeza gawio kwa Serikali kutoka Sh500 milioni hadi Sh8.4 bilioni, hatua inayoonesha kuongezeka kwa tija katika usimamizi na matumizi ya mtaji wa umma.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ojambi Didas Masaburi, wakati wa kikao cha kamati kilichofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo wajumbe walipata fursa ya kutathmini majukumu, muundo wa kiutendaji na changamoto zinazoikabili benki hiyo.

Masaburi amesema kamati hiyo ina wajibu wa kuhakikisha taasisi zinazopokea mitaji ya umma zinalinda uwekezaji huo, kuukuza na kuongeza tija kwa manufaa ya Watanzania. Ameeleza kuwa TADB imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na mwaka 2015, ilipokuwa katika mazingira magumu yaliyohatarisha kuendelea kwa shughuli zake.

Amesema pamoja na changamoto hizo, benki hiyo imefanikiwa kulinda mtaji wa Sh60 bilioni uliowekezwa na Serikali na kuongeza uwezo wake wa kuchangia mapato ya Serikali kupitia gawio.

Akizungumzia hatua za kusogeza huduma karibu na wakulima, benki hiyo imefungua ofisi nane za kanda katika mikoa ya Kagera, Ruvuma na Kigoma kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuwawezesha wakulima wadogo kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Ismail Andulile, amesema kamati hiyo imeitaka benki kuhakikisha mikopo inawafikia wakulima wadogo, hususan wanaoishi vijijini, akieleza kuwa kuwapatia huduma za kifedha kuanzia ngazi ya chini kutasaidia kuboresha shughuli za kilimo, kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wao.

Kwa upande wake, Ng’ambi amesema benki hiyo imepokea ushauri uliotolewa na kamati na kuahidi kuufanyia kazi, akibainisha kuwa suala la kuwafikia wakulima wadogo na wananchi wanaohitaji mikopo ya kilimo limekuwa miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele. Ameongeza kuwa TADB itaendelea kushirikiana na benki za biashara, ambazo ni wadau muhimu katika kusambaza huduma za kifedha, huku ikiimarisha mawasiliano na ushirikiano nao ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa mikopo nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button