Jeshi la Akiba Uvinza wasisitizwa mapambano dhidi ya uhalifu

KIGOMA: MKUU wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Mtela Mwampamba, amewaasa wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Akiba wilayani humo kuwa mstari wa mbele katika mapambano mbalimbali ikiwemo dhidi ya vitendo vya kihalifu.
Akizungumza wilayani humo Novemba 7, 2026 wakati akifunga mafunzo hayo kwa wahitimu 45 yaliyofanyika katika Kijiji cha Kandaga, Mwampamba amesema anaamini kupitia mafunzo hayo wahitimu hao watakuwa imara kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Niwapongeze kwa kuhitimu mafunzo haya lakini zaidi mnapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha vitendo vyote vya kihalifu ndani ya wilaya yetu na maeneo mengine havipati nafasi kwa maslahi mapana ya taifa letu,”amesema Mwampamba.
Aidha, amevitaja baadhi ya vitendo hivyo vya kihalifu ambavyo kwa nyakati tofauti vimekuwa vikijitokeza katika Wilaya hiyo kuwa ni pamoja na visasi vinavyotokana na visingizio vya uwepo wa imani za vitendo vya kishirikina na kusababisha baadhi ya watu kuchomewa nyumba zao.

Eneo jingine ambalo Mkuu wa Wilaya huyo amewatama wahitimu hao wa Jeshi la Akiba kwenda kukusimamia ni pamoja na Mapambano dhidi ya vitendo vya uwepo wa biashara ya pombe haramu wilayani humo ambavyo kwa namna moja au nyingine vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya wilaya hiyo na Mkoa kwa ujumla.
Amesema endapo wahitimu hao watatumia mafunzo waliyoyapata kwa weledi, nidhamu na uzalendo watakuwa wametimiza kikamilifu wajibu wao wa kulinda maisha na mali za wananchi pamoja na kudumisha amani na utulivu katika Wilaya hiyo ya Uvinza.



