Gofu yafungua milango ya ushirikiano wa biashara

ZANZIBAR: KAMPUNI ya Vodacom imeendelea kutumia mchezo wa gofu kuunganisha viongozi wa biashara, maafisa watendaji wakuu (CEO), wanadiplomasia na wadau wa sekta mbalimbali kupitia udhamini na ushiriki wake katika mashindano ya CEO Golf Tournament 2026.

Mashindano hayo yalifanyika Septemba 26, 2026, katika viwanja vya Sea Cliff Golf Course, Zanzibar, yakishirikisha zaidi ya wachezaji 80 kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali ya Afrika, yakiwemo Kenya, Uganda, Zambia, Malawi, Afrika Kusini na Nigeria.

Wachezaji kutoka Kenya, Thomas Mwangi na Caroline Muigai, walitwaa ubingwa wa jumla kwa wanaume na wanawake mtawalia katika mashindano hayo yaliyochezwa kwa mfumo wa Stableford kwenye mashimo 18.

Mwangi alitwaa ubingwa wa jumla kwa wanaume baada ya kukusanya pointi 40, huku Muigai akiibuka mshindi kwa wanawake kwa kupata pointi 41.

Katika Division A, Patrick O’Rourke alishinda nafasi ya kwanza, huku Ernest Sengeu akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 31.

Kwa upande wa Division B, Thagaran Govender alitwaa ushindi kwa pointi 39, akifuatiwa na Gregory Eayrs aliyepata pointi 38.

Katika Division C, Abbas Simkoko aliibuka mshindi kwa pointi 40, huku Joseph Sayi akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 37.

Kwa upande wa wanawake, Salome Gakere alishinda kwa pointi 36, huku Vicky Elias akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 35, sawa na Maryanne Mugo, lakini akashinda kwa kutumia mfumo wa countback.

Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema kampuni hiyo inajivunia kuunga mkono mashindano yanayounganisha michezo na jumuiya ya wafanyabiashara.

“Tunafurahi kudhamini na kushiriki mashindano ya CEO Golf Tournament kwa sababu gofu si mchezo pekee, bali ni jukwaa linalowakutanisha watu, mawazo na fursa,” alisema Kamando.

Alisema mashindano hayo yanatoa mazingira rafiki kwa viongozi wa biashara kutoka sekta mbalimbali kukutana, kubadilishana mawazo na kujenga mahusiano ya kikazi yanayoweza kufungua fursa za ushirikiano.

Kamando alisema pia mashindano hayo yana mchango katika kukuza utalii Zanzibar, akibainisha kuwa matukio ya kimataifa ya michezo yanaifanya Zanzibar kufahamika zaidi kwa wageni ambao wanaweza kurejea kwa shughuli za utalii na biashara.

“Tunajivunia kushiriki katika kuitangaza Zanzibar kama kituo cha biashara, utalii na michezo. Matukio kama haya yanaongeza thamani si kwa washiriki pekee, bali pia kwa uchumi kiujumla,” alisema.

Alisema ushiriki wa Vodacom Tanzania katika majukwaa kama CEO Golf Tournament unaipa kampuni hiyo fursa ya kukutana na viongozi wanaofanya maamuzi katika sekta ya biashara, kusikiliza mahitaji yao na kujadili namna teknolojia inavyoweza kusaidia biashara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Kupitia ushiriki huo, Vodacom Tanzania inaendelea kutumia majukwaa ya michezo kujenga mahusiano na viongozi wa makampuni, kuendeleza mazungumzo ya kibiashara na kuchochea fursa za ushirikiano katika mazingira ya biashara yanayozidi kutegemea teknolojia na huduma za kidijitali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button