Makonda ataka michezo itumike elimu utunzaji misitu

MOROGORO; WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema michezo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu na mazingira, kwani wanapoweza kuona na kunufaika na rasilimali hizo.

Makonda, amesema hayo  Oktoba 3, 2026 wakati wa ziara yake eneo la mashindano ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 katika  Shamba la Miti Morogoro, ambapo pia alitembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kupata maelezo kuhusu shughuli za uhifadhi zinazotekelezwa na wakala huo  .

Waziri Makonda amesema mashindano yanayofanyika katika mazingira ya misitu yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza kwa vitendo kuhusu thamani ya misitu na umuhimu wa kuilinda.

“Ni jambo la kujifunza kwa kuona, ukijifunza kwa vitendo unapata fursa kubwa zaidi ya kuelewa,” amesema Makonda.

Makonda amesema kuwa misitu ina mchango muhimu katika maisha ya wananchi, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa mvua na mazingira bora ya kuishi, hivyo jamii inapaswa kuendelea kunufaika nayo na kuzilinda rasilimali hizo.

Kwa kutambua umuhimu huo , amewahimiza  Watanzania kuwa walinzi wa misitu kwa kutambua thamani yake na kushiriki kikamilifu katika kuilinda dhidi ya uharibifu.

“ Manufaa yanayotokana na misitu yanaweza kuendelea kupatikana iwapo rasilimali hizo zitatunzwa kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Makonda.

Kwa upande wake, Ofisa Utalii wa TFS, Salome Kivuyo amesema Wakala huo unaendelea kuwashirikisha wadau na wafadhili katika kuendeleza michezo ndani ya maeneo ya misitu kwa kuzingatia taratibu za uhifadhi.

Kivuyo amesema kuwa michezo hiyo ni pamoja na  mbio za baiskeli, pikipiki na marathon, kwa lengo la kuunganisha michezo na uhifadhi wa mazingira.

“Tunawakaribisha wadau mbalimbali waje tushirikiane katika kuleta michezo ndani ya misitu yetu, ili kuwapa Watanzania fursa ya kufurahia michezo hiyo, huku wakijifunza, kutambua na kuthamini thamani ya misitu na umuhimu wa kuilinda,” amesema Kivuyo.

Akielezea mashindano hayo amesema yameandaliwa vema na kufanyika katika mazingira ya Shamba la Miti Morogoro, na kwa kuunganishwa michezo na uhifadhi kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ikiwa na kukuza michezo na utalii.

Kivuyo amesema kuwa Mashindano ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 yanayofanyika  Shamba la Miti Morogoro, linalosimamiwa na TFS, yamekuwa fursa ya kuunganisha michezo, uhifadhi, utalii na elimu ya mazingira.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button