Lake Victoria Marathon kufanyika Nov.15

MWANZA; Mashindano ya riadha ya Lake Victoria Marathon yanatarajiwa kufanyika Novemba 15, mwaka huu, jijini Mwanza, yakilenga kuhamasisha utunzaji wa Ziwa Victoria, kuimarisha afya za wananchi na kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya watoto njiti Kanda ya Ziwa.
Mratibu wa mashindano hayo, Hilda Viggo, amesema msimu wa sita wa mashindano hayo, umejikita kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa Ziwa Victoria kwa lengo la kulinda mazingira na kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka ziwa hilo.
Hilda amesema mashindano hayo pia yanalenga kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili.
Amesema mashindano hayo yatakuwa na vipengele vinne vya mbio, ambavyo ni kilomita 2.5 zinazojulikana kama Kids Challenge, kilomita 5, kilomita 10 zinazojulikana kama Corporate Run, pamoja na kilomita 21 za Half Marathon.
Ameongeza kuwa mashindano ya mwaka jana yalishirikisha zaidi ya watu 2,800, huku mwaka huu waandaaji wakilenga kufikisha washiriki wasiopungua 3,000.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza, Edwin Ngonyani, amesema chama hicho kimejipanga kuhamasisha wanariadha na wananchi kushiriki kwa wingi katika mashindano hayo.
“Tumeguswa na mpango wa mashindano haya wa kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati. Tunawahimiza wananchi kujisajili mapema ili kuongeza idadi ya washiriki na kuhakikisha mashindano yanafanikiwa,” amesema Ngonyani.
Naye, Meneja Biashara wa Mixx by Yas, Charles Elisante, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na waandaaji pamoja na serikali katika kuhakikisha watoto njiti wanapata msaada unaohitajika.



