Coop Bank yaunga mkono Kongamano la SACCA 2026

DAR ES SALAAM: BENKI ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) imetangaza ushirikiano wa kimkakati na Shirikisho la Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Afrika (ACCOSCA) pamoja na Chama Kikuu cha Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) katika kuunga mkono Kongamano la SACCA 2026, linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 11 hadi 16, 2026.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 300 kutoka zaidi ya nchi 35 kwa lengo la kujadili maendeleo ya vyama vya akiba na mikopo (SACCOS), kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuimarisha sekta hiyo barani Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah, amesema ushiriki wa benki hiyo unaakisi dhamira yake ya kuimarisha uchumi wa ushirika kwa kutoa suluhisho za kifedha zitakazowezesha SACCOS kukua, kuongeza ufanisi wa shughuli zake na kuboresha huduma kwa wanachama.

Amesema benki hiyo, inayomilikiwa kwa asilimia 51 na vyama vya ushirika, inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusaidia maendeleo ya sekta ya ushirika nchini kupitia huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wanaushirika.

Ng’urah ameeleza kuwa SACCOS zina nafasi muhimu katika mfumo wa uchumi wa ushirika nchini, hususan katika kuchangia mitaji na kuimarisha shughuli za kiuchumi za wanachama. Ameongeza kuwa vyama hivyo vina mchango mkubwa katika uwekezaji wa mitaji ikilinganishwa na baadhi ya makundi mengine ya vyama vya ushirika, yakiwemo vyama vya ushirika vya mazao na kilimo.

Katika kongamano hilo, Coop Bank inatarajia kuonesha bidhaa na huduma zake mbalimbali za kifedha zinazolenga kuwawezesha wanachama wa vyama vya ushirika, wateja na wananchi kwa ujumla kupata mitaji, kukuza biashara na kuongeza uwekezaji.

Huduma hizo pia zinalenga kusaidia ukuaji wa biashara ndogo na za kati, pamoja na kuchochea maendeleo ya mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanaushirika.

Akizungumzia upatikanaji wa mikopo, Ng’urah amesema benki hiyo imeweka kipaumbele katika kutoa mikopo kwa masharti nafuu kwa vyama vya ushirika, ikiwa ni pamoja na baadhi ya mikopo yenye viwango vya riba vya tarakimu moja.

Amesema viwango hivyo ni tofauti na viwango vingi vya soko ambavyo mara nyingi huwa katika tarakimu mbili, hatua inayolenga kupunguza gharama za mikopo na kuwawezesha wanaushirika kupata fedha za kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Muungano wa SACCOS Tanzania, Hassan Nyone, amesema kongamano hilo ni fursa muhimu kwa viongozi, watendaji, wanachama wa SACCOS, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa serikali kujadili mikakati ya kuimarisha vyama vya akiba na mikopo barani Afrika.

Nyone amesema ushiriki wa Coop Bank kama mshirika rasmi wa huduma za kibenki katika kongamano hilo utasaidia kuimarisha mahusiano kati ya benki hiyo na SACCOS za Afrika, kuwezesha ubadilishanaji wa uzoefu na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kifedha.

Ameongeza kuwa maendeleo ya SACCOS nchini Tanzania yana umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi jumuishi na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hususan katika kupanua fursa za kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.

Amesema kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa la kubadilishana maarifa, kujenga mitandao ya ushirikiano na kuandaa mikakati ya kukabiliana na changamoto za uendeshaji zinazozikabili SACCOS, huku zikitumia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta ya fedha.

Kupitia kongamano hilo, wadau wanatarajia kuimarisha ushirikiano wa kifedha na kitaasisi utakaosaidia kuongeza uwezo wa SACCOS kutoa huduma bora kwa wanachama wao na kuchangia maendeleo ya kiuchumi katika jamii.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Cash earning job to earns more than $700 per day. getting paid weekly more than $3500 or more simply doing easy work online. no special skills required for this job and regular earning from this are just awesome. all you need is 2 hrs a day for this job and earning are awesome. every person can get this by follow details here…

    THIS→→→→ http://Www.Payathome1.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button