Waiomba serikali iwape fursa ujenzi

DAR ES SALAAM; Chama cha Mafundi Rangi na Ujenzi Tanzania (CHAMARAUTA) kimeiomba Serikali na wadau wa sekta ya ujenzi kuwapa mafundi nchini fursa za kushiriki katika miradi mbalimbali ya ujenzi ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Mwenyekiti wa CHAMARAUTA, Juma Chakusaga, ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kusitishwa kwa mkataba wa kibiashara kati ya chama hicho na kampuni ya AB Company Ltd. Aidha, amezitaka kampuni nyingine na wawekezaji katika sekta ya ujenzi kujitokeza na kushirikiana na chama hicho katika kuwawezesha mafundi kupata fursa za kiuchumi.

Chakusaga amewahimiza mafundi rangi na ujenzi nchini kujiunga na chama hicho ili kuimarisha umoja na mshikamano, akieleza kuwa kupitia umoja huo wataweza kukutana, kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho kwa pamoja.

Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni kufanya kazi katika mazingira hatarishi, kukosa mikataba rasmi ya kazi na uhitaji wa elimu zaidi ya kitaalamu ili kuboresha utendaji wao.

Ameeleza kuwa kujiunga na CHAMARAUTA kutawapa mafundi jukwaa la kutetea maslahi yao, kupata elimu ya kuwaongezea ujuzi na kuimarisha uwezo wao wa kupata ajira pamoja na fursa za kutoa huduma za ujenzi.

Ameongeza kuwa mafundi wakiwa na umoja imara, itakuwa rahisi zaidi kutafuta fursa za kazi, kujadiliana na kampuni na kujenga ushirikiano na wawekezaji katika sekta hiyo.

Aidha, Chakusaga amezitaka kampuni zinazozalisha vifaa vya ujenzi na wawekezaji wengine kushirikiana na chama hicho kupitia uwekezaji na matangazo ya biashara zao, akibainisha kuwa ushirikiano huo utasaidia kuimarisha shughuli za chama na kuongeza uwezo wake wa kuwahudumia mafundi nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button