Teknolojia kuibua fursa mpya vikundi vya upatu

DAR ES SALAAM: Utamaduni wa Watanzania wa kuweka akiba kwa pamoja kupitia vikundi vya upatu unatarajiwa kupata msukumo mpya kufuatia uzinduzi wa huduma ya MCHEZO kupitia M-Pesa, inayolenga kurahisisha usimamizi wa michango na kuimarisha uwazi miongoni mwa wanachama.

Kwa miaka mingi, upatu umekuwa sehemu ya maisha ya jamii, ukiwawezesha watu wenye kipato tofauti kuunganisha nguvu zao za kifedha, kusaidiana kutimiza malengo na kukabiliana na mahitaji mbalimbali ya maisha. Kupitia utaratibu huo, wanachama huchangia fedha kwa vipindi maalumu na kupokezana zamu ya kupokea fedha zinazokusanywa.

Hata hivyo, pamoja na mchango wake katika kujenga utamaduni wa kuweka akiba, usimamizi wa fedha taslimu na kumbukumbu kwa njia za kawaida umekuwa ukihitaji uaminifu, ufuatiliaji na mawasiliano ya karibu ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza miongoni mwa wanachama.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Vodacom Tanzania PLC imezindua MCHEZO, huduma ya kidijitali inayowawezesha wanachama wa vikundi vya upatu kusimamia michango, kufuatilia malipo na kupata taarifa za shughuli za vikundi kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS).

Kupitia huduma hiyo, waandaaji wa vikundi wanaofahamika kama vijumbe wataweza kuanzisha vikundi, kupanga viwango na ratiba za michango, kuwaalika wanachama na kufuatilia malipo, huku wanachama wakichangia kupitia akaunti zao za M-Pesa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo Novemba 10, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa wa Vodacom Tanzania, Tulisindo Mlupilo, alisema MCHEZO inalenga kuendeleza utaratibu wa jadi wa kuweka akiba kwa pamoja kwa kutumia teknolojia inayorahisisha usimamizi wa shughuli za vikundi.

Alisema upatu umeendelea kuwa nyenzo ya kijamii inayowaunganisha Watanzania katika kuweka akiba na kusaidiana kufikia malengo yao ya kifedha, hivyo matumizi ya teknolojia yanaweza kurahisisha zaidi ushiriki na usimamizi wake.

“Kwa muda mrefu, upatu umekuwa ukiwapa Watanzania fursa ya kuweka akiba kwa pamoja na kusaidiana kutimiza malengo yao ya kifedha. Kupitia MCHEZO, tunaupeleka utaratibu huu uliozoeleka katika mazingira ya kidijitali,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki kwa Wateja Binafsi wa ABSA, Ndabu Lilian Swere, alisema ushirikiano katika huduma hiyo unaunganisha teknolojia na utaalamu wa kibenki ili kuboresha usimamizi wa akiba za vikundi.

Naye Mkurugenzi wa Afropavo Limited, Rwebu Mtahaba, alisema mfumo huo utasaidia kuweka kumbukumbu za michango kidijitali, kutoa taarifa kwa SMS na kupanga malipo kulingana na kanuni zilizokubaliwa na wanachama.

Huduma hiyo ni matokeo ya ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania, Afropavo Limited na ABSA Bank, kila mmoja akitoa mchango wake katika teknolojia, uendeshaji wa huduma na utaalamu wa kibenki.

Kabla ya uzinduzi, vijumbe walishiriki katika majaribio ya huduma hiyo na kutoa maoni yaliyosaidia kuboresha mpangilio wa malipo, ada za usimamizi na ukomo wa idadi ya wanachama.

Katika wiki 12 za mwanzo, Vodacom inatarajia kutoa elimu kuhusu matumizi ya MCHEZO kupitia majukwaa ya kidijitali, shughuli za kijamii na mawasiliano ya moja kwa moja ili kuwafikia wanaotumia upatu na wanaotaka kuanzisha vikundi vipya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button