Vijana 300 Muleba kupata fursa kilimo cha kahawa

MULEBA: Zaidi ya vijana na wanawake 300 wanatarajiwa kupata fursa za ajira na kipato kupitia kilimo cha kahawa katika Shamba la Vijana na Wanawake la Makongora, wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia sekta ya kilimo badala ya kutegemea ajira rasmi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), Dk. Nyamahanga amesema maandalizi ya shamba hilo yameanza kwa kusafisha mashamba na kuchonga barabara yenye urefu wa kilometa 20.

Amesema kila kijana anaweza kupata mauzo ya kahawa yenye thamani ya hadi Sh milioni nane kwa msimu, iwapo atazingatia kanuni bora za kilimo. Kwa mujibu wake, shamba hilo lina uwezo wa kuvuna mara mbili kwa mwaka.
Aidha, amesema hekari 28 ambazo bado hazijagawiwa zitatolewa kwa vijana wengine wa kata hiyo, hatua itakayopanua mradi kutoka ngazi ya kijiji hadi kata.

Mratibu wa BBT Wilaya ya Muleba, Daudi Kingu, amesema mafunzo kwa wanufaika yataanza Novemba 9, 2026, yakihusisha kilimo bora, matumizi ya teknolojia, umwagiliaji, usimamizi wa biashara, masoko na upatikanaji wa mikopo.
Amesema maandalizi mengine ni pamoja na kuweka miundombinu ya maji, kujenga ofisi ya AMCOS na kutoa huduma za ugani ili kuwawezesha vijana kuendesha shughuli za kilimo kwa tija.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Halmashauri ya Muleba, Charles Ntaki, amesema shamba hilo lilianzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa kahawa na kuinua uchumi wa vijana.

Amesema mradi huo pia umeanza kuvutia watu binafsi na wawekezaji kuanzisha mashamba makubwa ya kahawa katika Kata ya Ruhanga.


