Mufindi yafungua fursa mpya uwekezaji misitu

IRINGA: Tanzania imeongeza msukumo wa kuwekeza katika uchakataji wa mazao ya misitu wilayani Mufindi, huku wadau wakisema hatua hiyo inaweza kuongeza thamani ya bidhaa, ajira na mapato yanayotokana na sekta hiyo.
Wadau wa sekta ya misitu wameiomba Serikali na Sekta Binafsi kuweka nguvu zaidi katika teknolojia za uchakataji, viwanda vya samani na uzalishaji wa bidhaa nyingine zinazotokana na mbao, badala ya kutegemea zaidi uuzaji wa mazao ya misitu bila kuongeza thamani.
Wakizungumza katika mkutano wa majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi ulioandaliwa na Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), wadau hao pia wameeleza changamoto zinazokabili sekta hiyo, zikiwemo ukosefu wa mitaji na mikopo nafuu, kodi na tozo, upatikanaji wa masoko na taratibu za vibali.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPSF, Deogratius Massawe, amesema ushirikiano kati ya Serikali na wafanyabiashara ni muhimu katika kutafuta suluhisho la changamoto hizo na kuweka mazingira yatakayowezesha uzalishaji na uwekezaji kukua.

Amesema TPSF itawasilisha mapendekezo ya wadau kwa taasisi husika za Serikali na kufuatilia hatua zitakazochukuliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema sekta ya misitu ina nafasi muhimu katika uchumi wa eneo hilo kupitia mapato ya halmashauri, ajira na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda.
Amesema uwekezaji zaidi katika uchakataji wa mazao ya misitu unaweza kuongeza manufaa yanayopatikana kutokana na rasilimali hizo, huku akisisitiza umuhimu wa matumizi endelevu ya misitu.
Mkutano huo wa Mufindi uliwakutanisha wawakilishi wa Serikali, taasisi za fedha, wawekezaji, wafanyabiashara, wazalishaji na wajasiriamali kujadili fursa za uwekezaji na namna ya kuboresha mazingira ya biashara katika sekta ya misitu.



