Benki ya Azania yajiweka mguu sawa AFCON 2027

DAR ES SALAAM; Watanzania wametakiwa kuweka utamaduni wa kujiwekea akiba ili ziweze kuwasaidua siku za usoni.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Biashara za Kiserikali wa Benki ya Azania, Samson Mahimbi wakati akizindua kampeni ya Piga Ndeefu yenye lengo la kuchochea shughuli za kiuchumi kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, yakitarajiwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi katika sekta za utalii, malazi, usafiri na huduma nyingine.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Dar es Salaam, amesema kampeni hiyo inalenga kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuchochea shughuli za kiuchumi zitakazowanufaisha Watanzania wakati wa maandalizi na kipindi cha mashindano ya AFCON 2027.
Mahimbi amesema kupitia kampeni hiyo, wateja watapata fursa ya kuweka akiba huku wakinufaika na riba pamoja na nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali.
Amesema wateja wanaweza kuanza kuweka akiba kwa kiasi cha shilingi 500,000 na kupata riba ya hadi asilimia 12 kwa mwaka, kwa mujibu wa masharti ya kampeni hiyo.
Aidha, zawadi zitakazotolewa kwa washindi ni pamoja na tiketi za kushuhudia mechi ya ufunguzi na fainali za AFCON 2027, simu janja, televisheni na fedha taslimu.
Kampeni ya Piga Ndeefu itaendelea hadi Julai 21, 2027, huku Benki ya Azania ikilenga kuwahamasisha Watanzania kutumia fursa hiyo kujiwekea akiba na kuimarisha uwezo wao wa kifedha.
Benki hiyo pia inalenga kupitia kampeni hiyo kuongeza fursa za upatikanaji wa mitaji kwa biashara katika sekta mbalimbali zitakazochangia shughuli za kiuchumi zinazohusiana na maandalizi na uendeshaji wa mashindano ya AFCON 2027.



