Tembo Queens waanza safari ubingwa Afrika

DAR ES SALAAM: Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu Tanzania (TAFF), limeanza maandalizi ya timu ya taifa ya wanawake, Tembo Queens, kwa ajili ya mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.
Akizungumza na DailyNews Digital, Ofisa Habari wa TAFF, Khalidi Msabaha, amesema kikosi hicho kimeanza maandalizi kwa kukusanya wachezaji kutoka mikoa mbalimbali nchini, hatua inayolenga kujenga timu yenye ushindani kabla ya mashindano hayo.
Amesema wachezaji hao kutoka Dar es Salaam, Songwe, Pwani na maeneo mengine walikutana kwenye Uwanja wa Uhuru kwa kambi ya awali ya wiki moja, ambako walipata mazoezi na mafunzo ya mchezo huo.
Msabaha amesema kikosi cha kwanza cha Tembo Queens tayari kipo na kwamba maandalizi ya hatua inayofuata yanasubiri uamuzi kuhusu ufadhili wa kambi kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Amesema shirikisho limeomba msaada huo kwa kuwa bajeti yake haitoshelezi kugharamia mahitaji yote ya kambi, hivyo wachezaji wataitwa tena kwa maandalizi zaidi baada ya kupata majibu kuhusu ombi hilo.



