EAC yataka viwanda vizalishe zaidi

DAR ES SALAAM: Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kuongeza uwekezaji katika viwanda na uchakataji wa malighafi ili kuacha kupoteza fursa za kiuchumi kwa kuuza bidhaa ghafi nje ya ukanda na baadaye kuagiza bidhaa zilizoongezwa thamani.
Wito huo umetolewa leo Dar es Salaam wakati wadau wa sekta ya umma na binafsi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wakijadili namna ya kuimarisha minyororo ya thamani katika sekta za ngozi, nguo na mafuta ya kula.
Mchumi mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Amedeus Mzee, amesema mafanikio ya juhudi za kuendeleza viwanda yanapaswa kupimwa kwa hatua zinazochukuliwa baada ya mikutano, ikiwemo kuongeza uzalishaji, kupanua masoko ya wakulima na kuhakikisha wazalishaji wanapata malighafi kwa wakati.

Amesema mazingira bora ya biashara yanahitajika ili viwanda viweze kuongeza uzalishaji, kuwekeza katika teknolojia na kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Mshauri wa biashara na sera wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Adrian Njau, amesema ukanda huo unaendelea kuagiza bidhaa nyingi zilizokamilika licha ya kuwa na uwezo wa kuzalisha baadhi ya malighafi zinazotumika katika utengenezaji wake.
Kwa mfano, amesema mwaka 2025 nchi za EAC ziliuza nje ngozi ghafi na iliyochakatwa kwa sehemu yenye thamani ya takribani dola milioni 46, lakini zikaagiza viatu, vipuri na bidhaa za ngozi zenye thamani ya takribani dola milioni 566.
Kwa mujibu wa Njau, tofauti hiyo inaonyesha fursa kubwa iliyopo katika kuongeza uchakataji wa ngozi ndani ya ukanda huo hadi kufikia utengenezaji wa viatu, mikoba na bidhaa nyingine zenye thamani kubwa.

Amesema changamoto zinazokabili viwanda ni pamoja na upatikanaji mdogo wa malighafi, mitaji, teknolojia na ujuzi, huku baadhi ya viwanda vikitumia sehemu ndogo ya uwezo wao wa uzalishaji.
Njau amezitaka nchi wanachama kuoanisha sera za biashara, ushuru, kanuni za asili ya bidhaa na mifumo ya ununuzi wa umma ili bidhaa zinazozalishwa ndani ya EAC zipate nafasi katika masoko ya nchi wanachama.
Amesema mahitaji ya sare za shule, viatu, mashuka ya hospitali na bidhaa nyingine zinazotumiwa na taasisi za umma yanaweza kuwa soko la uhakika kwa wazalishaji wa ndani iwapo sera zitaweka mazingira rafiki kwa bidhaa zinazotengenezwa ndani ya ukanda huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Frank Dafa, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kukuza uzalishaji wa ndani, lakini bado kuna pengo kati ya uzalishaji wa malighafi na uwezo wa kuzichakata kuwa bidhaa zilizokamilika.

Amesema mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kufikia tani 720,000 kwa mwaka, wakati uzalishaji wa ndani ni takribani tani 302,000, hali inayosababisha upungufu wa zaidi ya tani 400,000 kwa mwaka.
CTI imependekeza kuimarisha uhusiano kati ya wakulima, wafugaji na viwanda, kuboresha teknolojia, ujuzi na miundombinu, pamoja na kuweka sera zitakazochochea uzalishaji na matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi.
Silvester Kazi, mjumbe wa kamati ya mradi huo, amesema nchi za Afrika Mashariki zinapoteza fursa za kiuchumi kwa kuuza mazao katika hali ghafi na baadaye kuagiza bidhaa zilizoongezwa thamani, ikiwemo nguo, viatu na mafuta ya kula.
Amesema lengo ni kuhakikisha sehemu kubwa ya ongezeko la thamani katika bidhaa hizo inafanyika ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki badala ya fedha na fursa za ajira kuelekezwa nje ya ukanda huo.



