CMAG yatambua hatua za Tanzania kuelekea maridhiano

NEW YORK, Marekani: Kundi la Mawaziri la Jumuiya ya Madola (CMAG) limetambua ushirikiano wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, pamoja na hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza mazungumzo ya kisiasa na maridhiano Zanzibar.

CMAG imesema hatua hizo ni msingi mzuri wa kuendeleza maendeleo zaidi katika mchakato huo.

Kauli hiyo imetolewa katika kikao cha 74 cha CMAG kilichofanyika Septemba 20, 2026, kwa njia ya dharura, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York.

Katika kikao hicho, CMAG ilifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa John Palamagamba Kabudi.

CMAG imetambua ushirikiano wa Tanzania na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu, mazungumzo ya hivi karibuni na vyama vya siasa pamoja na hatua kuelekea maridhiano Zanzibar.

Hatua hivyo, kundi hilo limesema bado kuna haja ya hatua zaidi katika kuendeleza mchakato shirikishi na unaoaminika wa vyama vya siasa.

Aidha, CMAG imesisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa kiraia, kisiasa na vyombo vya habari, kuhakikisha taratibu za haki, kwa wakati na uwazi katika mashauri yaliyosalia, pamoja na kuwepo kwa mifumo inayoaminika ya uwajibikaji, marekebisho na fidia stahiki kwa walioathirika.

CMAG pia imeihimiza Serikali ya Tanzania kuweka tarehe ya mapema kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, ambayo itamwezesha kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine.

Pamoja na hatua hizo, CMAG imekubali Tanzania kuendelea kubaki kwenye Ajenda Rasmi (Formal Agenda) ya kundi hilo.

Katika kikao hicho, CMAG pia ilifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Adonia Ayebare, na kuamua Uganda pia iendelee kubaki kwenye Ajenda Rasmi.

CMAG ni chombo cha Jumuiya ya Madola kinachofuatilia na kuunga mkono utekelezaji wa misingi ya kisiasa ya Jumuiya hiyo, ikiwemo demokrasia, utawala wa sheria, haki za binadamu na utawala bora.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button