Kigogo Ghana kortini Uingereza kupinga hukumu ya Dola mil. 14.9

Adai nyaraka zilizotumika kupata hukumu ya awali zilipatikana kwa njia ya udanganyifu

ACCRA, GHANA: Mjasiriamali maarufu, mfanyabiashara na aliyekuwa mgombea urais nchini Ghana, Nana Kwame Bediako, amerudi katika Mahakama Kuu ya Uingereza kupinga hukumu ya dola milioni 14.9 iliyotokana na mgogoro wa muda mrefu wa uendelezaji wa mali nchini Ghana.

Anadai kuwa nyaraka zilizotumika kupata hukumu ya awali zilipatikana kwa njia ya udanganyifu.

Bediako, anayejulikana zaidi kama Cheddar, ni mwanzilishi wa kampuni ya Kwarleyz Group, yenye shughuli za kibiashara katika sekta za uendelezaji wa milki (real estate), ujenzi, nishati na ukarimu. Pia alianzisha kampuni ya milki ya Wonda World na taasisi ya hisani ya New Africa Foundation.

Aidha, aligombea katika uchaguzi wa urais wa Ghana mwaka 2024 akiwa mmoja wa wagombea urais wenye umri mdogo zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Bediako anatafuta kubatilisha hukumu ya Mahakama Kuu ya Uingereza ya Januari 2025 iliyomwamuru kulipa dola milioni 14.9 kwa kampuni ya Cola Holdings Limited, ambayo ni kampuni ya uwekezaji wa mali ya familia ya Cola yenye makao yake jijini London.

Hukumu hiyo ilifuatia mgogoro kuhusu mkopo wa dola milioni 18 uliopatikana kufadhili ujenzi wa No. 1 Oxford Street, jengo la ghorofa lenye nyumba 108 za huduma (serviced apartments) jijini Accra. Sasa Bediako anapinga hukumu hiyo, akidai kuwa hati ya fidia (deed of indemnity) iliyotumika kuthibitisha dhima yake ilikuwa na saini ambayo hakuidhinisha wala kuiweka.

Kesi hiyo inahusu mradi wa No. 1 Oxford Street, jengo lililopo Accra lenye nyumba 108 za huduma. Mradi huo ulitokana na uhusiano wa kibiashara kati ya Bediako na Azad Cola, huku ikiripotiwa kuwa wawili hao wamefahamiana tangu karibu mwaka 2009.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, familia ya Cola ilipata mkopo wa dola milioni 18 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) ili kufadhili ujenzi huo. Mkopo huo ulipodaiwa mwezi Aprili 2023, familia ya Cola ilisisitiza kuwa Bediako alikuwa na wajibu wa kulipa nusu ya kiasi kilichokuwa kikidaiwa.

Hatua zao za kisheria zilizofuata zilisababisha hukumu ya dola milioni 14.9 dhidi ya Bediako mwezi Januari 2025.

Hata hivyo, katika madai mapya yaliyowasilishwa mwishoni mwa Oktoba 2026, Bediako amepinga uhalali wa nyaraka zilizotumika katika mashauri ya awali. Timu yake ya wanasheria inasisitiza kuwa saini iliyokuwa kwenye hati ya fidia haikuwa yake na kwamba hana ufahamu wa jinsi ilivyowekwa kwenye waraka huo.

Nyaraka hizo zinaeleza zaidi kuwa Bediako alikuwa nchini Nigeria mnamo Januari 18, 2018, tarehe ambayo waraka huo unadaiwa kusainiwa ofisini kwake jijini Accra.

Wanasheria wake wamedokeza kuwa huenda nakala ya kielektroniki ya saini yake ilitumika bila yeye kujua wala kutoa idhini.

SOMA: GHANA : Matokeo ya uchaguzi wa rais yathibitishwa

Pia wameibua maswali kuhusu nafasi ya aliyekuwa msaidizi wake mkuu, Reginald Sittie, ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano wa kikazi na pande zote mbili. Madai ya Bediako mahakamani yanadai kuwa Azad Cola alimpa Sittie zawadi ya saa aina ya Rolex katika majira ya kuchipua ya mwaka 2018.

Ingawa Bediako amesisitiza kuwa hadai kuwepo kwa rushwa, timu yake ya wanasheria inahoji kuwa zawadi hiyo inaibua maswali kuhusu asili ya uhusiano wao na iwapo Sittie alikuwa akifanya kazi kwa uhuru katika masuala yaliyowahusu wafanyabiashara hao wawili.

Aidha, timu ya wanasheria ya Bediako imehoji iwapo kampuni ya Cola Holdings ilijua, au ilipuuza kwa uzembe, kasoro zinazodaiwa kuwepo katika nyaraka zilizowasilishwa mahakamani.

Mfanyabiashara huyo anataka hukumu ya awali itenguliwe na pia anadai fidia kwa kile anachokielezea kuwa ni hasara kubwa iliyotokana na hukumu hiyo ya awali.

Mgogoro huo umevutia hisia kutokana na hadhi ya wahusika. Bediako ni mtu anayefahamika vyema katika ulingo wa biashara na siasa nchini Ghana, akiwa amejijengea jina kubwa kibiashara kabla ya kuingia katika kinyang’anyiro cha urais wa nchi hiyo mwaka 2024.

Hatua yake ya kupinga hukumu hiyo inaibua maswali mapana kuhusu uwajibikaji wa kibiashara, uwekaji wa nyaraka, na ulinzi wa maslahi ya kibiashara katika mikataba ya uwekezaji wa kimataifa.

Kampuni ya Cola Holdings imekanusha vikali madai hayo. Akiiwakilisha kampuni hiyo, Lawrence Cartier amesema familia hiyo inakanusha kabisa madai hayo na inakusudia kuwasilisha utetezi wa kina katika Mahakama Kuu ya Uingereza.

Katika hatua nyingine, Cola Holdings inafuatilia umiliki wa No. 1 Oxford Street kupitia taratibu za ufilisi (receivership) nchini Ghana. Jengo hilo, lililofunguliwa mwanzoni mwa janga la UVIKO-19 (COVID-19), linaripotiwa kusitisha kupokea wateja wapya (reservations).

Mashauri haya ya hivi karibuni yataipa Mahakama Kuu fursa ya kuzingatia madai ya Bediako na kuamua iwapo hukumu ya awali itaendelea kusimama.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button