Tanzania yatakiwa kuweka tarehe ziara ya Katibu Mkuu

NEW YORK: Tanzania imetakiwa kuweka tarehe ya mapema kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola nchini, ili kufanya mazungumzo na Rais Dk Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine.
Aidha, Kundi la Mawaziri la Jumuiya ya Madola (CMAG) limekubali Tanzania kuendelea kubaki kwenye Ajenda Rasmi (Formal Agenda) ya kundi hilo.
Hatua hiyo imefikiwa katika kikao cha 74 cha CMAG kilichofanyika Septemba 20, 2026, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York.
CMAG ilifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa John Palamagamba Kabudi.
Kundi hilo lilitambua ushirikiano wa Tanzania na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, mazungumzo ya hivi karibuni na vyama vya siasa pamoja na hatua kuelekea maridhiano Zanzibar, likisema hatua hizo ni msingi mzuri wa kuendeleza maendeleo zaidi.



