Mzumbe yaongeza fursa elimu ya juu

MOROGORO: CHUO Kikuu Mzumbe kimesema ongezeko la idadi ya wanafunzi ni miongoni mwa viashiria vya ukuaji wake wa kimkakati na upanuzi wa fursa za elimu ya juu nchini, huku kikiendelea kuboresha mitaala ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Mwegoha, amesema hayo Oktoba 22, 2026, wakati akiwasilisha hotuba yake kwa Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, katika Mahafali ya 25 yaliyofanyika Kampasi Kuu ya Morogoro, Mzumbe, eneo la Maekani, wilayani Mvomero.

Profesa Mwegoha amesema katika kipindi cha miaka mitatu, idadi ya wanafunzi katika Kampasi Kuu ya Morogoro, Ndaki ya Dar es Salaam na Ndaki ya Mbeya imeongezeka kutoka 15,086 katika mwaka wa masomo 2023/2024 hadi 17,035 mwaka 2025/2026.

Amesema ongezeko hilo linaonesha hatua zinazopigwa na chuo katika kupanua fursa za elimu ya juu, huku kikizingatia uwiano wa kijinsia katika upatikanaji wa elimu.

Kwa mujibu wa Profesa Mwegoha, wanafunzi hao wanajumuisha wanaume 8,595, sawa na asilimia 50.45, na wanawake 8,440, sawa na asilimia 49.55.

Amesema kati ya wanafunzi hao, 13,920 wanasoma Shahada za Awali, 1,437 Shahada za Umahiri na 57 Shahada za Uzamivu (PhD).

“Ingawa bado tuna jukumu la kuongeza idadi ya wanafunzi, ukuaji huu na uwiano wa kijinsia ni hatua muhimu katika kupanua fursa za elimu ya juu,” amesema Profesa Mwegoha.

Katika hatua nyingine, amesema chuo hicho kinaendelea kufanya mapitio ya mitaala ya masomo ili kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya soko la ajira, vipaumbele vya maendeleo ya Taifa na maelekezo ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Amesema mapitio hayo yanalenga kuimarisha programu za masomo na kuwaandaa wahitimu wenye maarifa na ujuzi unaowawezesha kuajirika, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Ameongeza kuwa jitihada hizo ni sehemu ya maandalizi ya wahitimu watakaoweza kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button