Rais Samia kuzindua Mji wa Serikali Okt.30
DODOMA: Uzinduzi rasmi wa majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma utafanyika Oktoba 30, 2026, ukiongozwa na Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo mjini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali imewekeza takribani Sh bilioni 700 katika ujenzi wa mji huo ambao umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wizara na taasisi za serikali.
Amesema ujenzi wa miundombinu hiyo ulianza mwaka 2021, ukiwa sehemu ya kuendeleza uamuzi wa Serikali wa kuhamishia shughuli zake Dodoma uliofikiwa mwaka 2016.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendeleza juhudi zilizoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujenga majengo ya kisasa yatakayoboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema Mji wa Serikali Mtumba una takribani kilometa 59 za barabara za lami pamoja na mifumo ya kisasa ya mawasiliano inayowezesha shughuli za Serikali kufanyika kwa njia ya mtandao.



