Wanafunzi KCMC watakiwa kuzingatia nidhamu, maadili

KILIMANJARO; Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Lazaro Mwanyasi, ameonya wanachuo wapya wa Chuo Kikuu cha Udaktari na Uuguzi cha KCMC mkoani Kilimanjaro wasijihusishe na vitendo vya uhalifu na kuwataka wazingatie maadili mema na nidhamu.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu ya ulinzi na usalama kwa wanachuo wa mwaka wa kwanza, Mwanyasi aliwahimiza kujitambua, kusimamia misimamo yao na kuzingatia misingi ya imani zao za dini, huku akiwataka kuepuka kufuata mikumbo ya watu wenye mienendo isiyofaa.

Mwanyasi alionya pia wanachuo hao dhidi ya kujihusisha na uanaharakati usiozingatia taratibu na kanuni za chuo, akiwataka kuelekeza nguvu zao katika masomo na kujenga msingi imara wa maisha yao ya baadaye badala ya kujiingiza katika makundi au shughuli zinazoweza kuvuruga masomo, nidhamu na amani chuoni.
Amewasisitiza kutokubali tamaa ya fedha na ushawishi wa makundi yasiyofaa kuwapeleka katika vitendo vya uhalifu, akibainisha kuwa fursa ya kupata elimu ya juu ni hatua muhimu inayohitaji uwajibikaji, nidhamu na matumizi sahihi ya muda, ili kufikia malengo yao ya kitaaluma na kimaisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto Mkoa wa Kilimanjaro, SSP Asia Matauka, aliwahimiza wanachuo hao kujitambua na kuthamini fursa waliyoipata ya kusoma katika chuo hicho.
Pia, aliwataka kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini matukio ya ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Naye Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Moshi, SP Juma Kabelwa, aliwasisitiza wanachuo hao kuzingatia usalama wao binafsi kwa kuepuka kutembea peke yao nyakati za usiku bila sababu za msingi.



