Serikali yatoa ufafanuzi fedha za El Nino
DODOMA; Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu Sh bilioni 730 zinazohusishwa na maandalizi ya kukabiliana na athari za El Niño, ikieleza kuwa fedha hizo si bajeti mpya iliyotengwa, bali ni jumla ya makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutekeleza shughuli za taasisi mbalimbali katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa kuzingatia bajeti zilizoidhinishwa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa leo Oktoba 25, 2026 mjini Dodoma.
Amesema Serikali imeandaa mpango wa taifa wa kujiandaa na kukabiliana na El Niño baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa utabiri wa uwezekano wa kutokea kwa El Niño yenye nguvu katika kipindi cha mwaka 2026/2027.
Amesema hali hiyo inaweza kusababisha mvua kubwa, mafuriko, maporomoko ya ardhi na magonjwa ya mlipuko, hivyo kuhitaji maandalizi ya mapema ili kulinda maisha na mali za wananchi.
Amesema mpango huo unahusisha ukarabati na uboreshaji wa barabara, madaraja na mitaro, pamoja na kulinda miundombinu ya afya, elimu, umeme, maji na mawasiliano.
Hatua nyingine ni ununuzi na uhifadhi wa chakula, maandalizi ya vifaa vya uokoaji na makazi ya muda kwa wananchi watakaolazimika kuhama maeneo yao endapo maafa yatatokea.
Ameeleza kuwa utekelezaji wake utahusisha wizara, idara, taasisi za Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na wananchi.
Aidha Msigwa amewataka wananchi kufuatilia taarifa za tahadhari zinazotolewa na TMA na mamlaka nyingine husika, na kuchukua hatua za kujikinga kulingana na maelekezo yatakayotolewa.



