Watanzania waaswa kulinda amani

DODOMA: MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesisitiza umuhimu wa Watanzania kudumisha amani na utulivu kwa kuepuka vitendo vya vurugu na ukiukwaji wa sheria, akiwataka wanaokuwa na malalamiko kutumia njia halali kuyawasilisha badala ya kuchochea migogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema mazingira ya amani ni muhimu katika kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kila siku na kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo bila vikwazo.
Amesema serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema dira hiyo inalenga kukuza uchumi wa Tanzania kutoka takribani dola bilioni 90 za Marekani kwa sasa hadi dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Ameeleza kuwa kufikiwa kwa malengo hayo kunahitaji wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali, biashara, kilimo, elimu na huduma za afya katika mazingira salama.
Akirejelea matukio ya Oktoba 29, 2025, Msigwa amesema tukio hilo linapaswa kuwa funzo kuhusu umuhimu wa kulinda umoja wa taifa na kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi zinaendelea.
Aidha, amesema Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kulinda wananchi, mali zao na mipaka ya nchi, akisisitiza kuwa kila mtu anapaswa kuheshimu sheria.
Amewataka vijana, hususan wanaotumia mitandao ya kijamii, kuchunguza taarifa wanazokutana nazo na kuepuka ujumbe unaochochea vurugu, akieleza kuwa vyombo husika vinafuatilia maudhui yanayochapishwa pamoja na vitendo vinavyoweza kuvunja sheria.



