Mbarawa aridhishwa ujenzi daraja la SGR Malagarasi

TABORA: WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa daraja la Malagarasi lenye urefu wa mita 460, linalojengwa katika reli ya kisasa (SGR) kipande cha Tabora hadi Kigoma.
Akizungumza wakati wa kukagua maendeleo ya mradi huo, Profesa Mbarawa alisema kazi zinaendelea katika maeneo mbalimbali na hakuna mkandarasi aliyesimamisha utekelezaji wa ujenzi wa reli hiyo.

Alisema licha ya mradi huo kuanza kutekelezwa hivi karibuni, hatua zilizofikiwa zinaonesha uwezekano wa kukamilika kwa wakati uliopangwa, mwaka 2029.

“Kwa wanaosema kazi haifanyiki, ninyi ni mashahidi. Tumeona kazi ya kuweka misingi ya madaraja na mifereji ya maji, ambayo ni muhimu kabla ya kutandika reli,” alisema.

Alieleza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya mradi huo na kuhakikisha wakandarasi wanalipwa kulingana na kazi zilizotekelezwa na kuthibitishwa kupitia hati za malipo.

Kipande cha Tabora hadi Kigoma kinakadiriwa kugharimu dola za Marekani bilioni 2.7, sawa na takribani Sh trilioni saba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Machibya Shiwa, alisema daraja la Malagarasi ni eneo muhimu katika mradi huo kutokana na ugumu wa ujenzi wake na muda unaohitajika kukamilisha kazi.

Alisema daraja hilo linahitaji misimu mitatu ya kazi na kwamba maendeleo ya jumla ya mradi yamefikia asilimia 12.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa maeneo yenye changamoto kubwa za kihandisi kutarahisisha utekelezaji wa hatua zinazofuata.

Mradi huo ukikamilika, utawezesha usafiri wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, kwa treni zinazotarajiwa kusafiri kwa kasi ya hadi kilomita 160 kwa saa, hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha usafiri nchini.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button