Watanzania wanne wanyakua tuzo Jumuiya ya Madola

LONDON, UINGEREZA: Watanzania wametangazwa kuwa miongoni mwa washindi 100 wa tuzo za heshima za vijana katika uongozi 2026 zilizoandaliwa na taasisi ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza huku mmoja wao akialikwa kuhudhuria hafla ya utoaji wa tuzo hizo katika Kasri la St James’s Palace, jijini London, Uingereza.
Taarifa iliyotolewa na QECT 100 Young Leaders Awards na kuchapishwa hivi karibuni kwenye tovuti rasmi ya taasisi hiyo imewataja Watanzania hao kuwa ni Editha Mshiu, Noely Mapunda, Suleiman Salum Suleiman na Julius Mbungo, ambaye alihudhuria hafla hiyo.
Vijana hao wametajwa miongoni mwa vijana 100 mahiri kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola wanaoleta mabadiliko chanya katika jamii zao.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, mpango huo unaadhimisha kumbukumbu ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa aliyekuwa Malkia wa Uingereza, Elizabeth II, na kuenzi imani yake ya muda mrefu katika uwezo wa vijana kuimarisha jamii na kujenga mustakabali wa Jumuiya ya Madola.

“Waliochaguliwa kupitia mchakato wa ushindani mkubwa kutoka kwa maelfu ya waombaji wanawakilisha kazi zenye matokeo chanya katika sekta za elimu na ajira, mazingira, chakula na kilimo, afya na ujumuishi. Juhudi zao zinashughulikia changamoto za haraka katika jamii zao huku zikichangia maendeleo ya dunia kwa ujumla,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika miezi ijayo, washindi hao watashiriki programu maalumu, fursa za kujifunza na shughuli mbalimbali za ushirikishwaji katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.
“Mwaka huu wa maadhimisho ya miaka 100 una umuhimu mkubwa. Kupitia kuanzishwa kwa QECT, Marehemu Malkia Elizabeth II aliweka urithi wa kudumu wa kusaidia viongozi vijana ambao kazi zao zinabadilisha maisha ya watu. Leo, dhamira hiyo inaendelea chini ya udhamini wa Mfalme wa Uingereza,” iliongeza taarifa hiyo.
Mbungo, ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Toolboksi na mjasiriamali aliyeanzisha programu ya huduma za magari ya Spana, alihudhuria hafla ya utoaji wa tuzo hizo jijini London kabla ya kutembelea Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Akiwa ameambatana na mke wake, Joyce Mbungo, mbunifu huyo alimweleza Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki, kuhusu mradi wake na mipango ya kuipanua biashara hiyo ili kuwafikia watu wengi zaidi.
Balozi huyo alimpongeza Mbungo kwa mafanikio hayo, akieleza kuwa kutambuliwa kwake ni mafanikio yanayoiletea Tanzania heshima na yanayoweza kumfungulia milango ya kupata wawekezaji wanaoaminika, washirika wa kibiashara na masoko mapana zaidi.
Alimtaka Mbungo kuendeleza mafanikio hayo kwa kuendelea kubuni suluhisho mpya, kuzingatia uadilifu na kuongeza uelewa wa umma kuhusu huduma zinazotolewa na kampuni yake.



