TBS yakutana na wadau kujadili viwango vya petroli

DAR ES SALAAM; Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekutana na wadau wa sekta ya petroli na bidhaa zake kujadili viwango vya petroli vilivyoboreshwa kwa lengo la kuimarisha ubora wa mafuta, kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza katika mkutano wa wadau hao jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango TBS, Nickonia Mwambene amesema mkutano huo unalenga kuwezesha wadau kuelewa viwango hivyo, ikiwemo mabadiliko ya baadhi ya vigezo na taratibu za utekelezaji wake.

Amesema viwango hivyo vimeandaliwa katika ngazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na vinapitia taratibu  zote ikiwemo  maoni ya wadau na wananchi kabla ya kupitishwa kuwa viwango vya kitaifa.

Ameeleza kuwa mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya nishati duniani na kikanda yameifanya mifumo ya viwango kuhusisha si tu ufanisi katika utendaji wa mafuta, bali pia masuala ya afya, uendelevu wa mazingira na ulinganifu wa masharti ya biashara ya kimataifa.

Amesema, majadiliano hayo pia yanalenga kuweka mwongozo wa utekelezaji na kipindi cha mpito katika sekta ya mafuta, kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazotumika, huku yakihakikisha kuwa mahitaji ya kitaifa yanaendana na mifumo ya kikanda bila kusababisha usumbufu katika soko au upatikanaji wa mafuta.

Amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha soko linapata mafuta yenye ubora unaotakiwa, huku mazingira yakilindwa na sekta ya nishati ikiendelea kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button