Katavi walenga elimu zaidi kupunguza udumavu

KATAVI; Serikali mkoani Katavi imewataka wadau na wataalamu wa lishe kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya teknolojia za uongezaji wa madini na vitamini kwenye vyakula, pamoja na uchakataji wa mazao ya mifugo, ili kuboresha lishe na kupunguza udumavu kwa watoto.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela, wakati wa siku ya tatu ya Maonesho ya Wiki ya Mwanakatavi, baada ya kutembelea kituo cha uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula na uongezaji wa thamani ya mazao ya mifugo wilayani Mpanda.
Msovela amesema matumizi ya mashine zinazotumika katika shughuli hizo bado ni madogo mkoani humo, huku wananchi wengi wakiwa na uelewa mdogo kuhusu umuhimu wake.

Amewataka wataalamu kuimarisha kampeni za elimu na hamasa mijini na vijijini ili wananchi wengi zaidi wanufaike na teknolojia hizo.
“Uwepo wa mashine hizi zinazosaidia uongezaji wa virutubishi na thamani ya mazao ya mifugo bado ni mdogo. Watu wengi bado hawana uelewa kuhusu mashine hizi. Hivyo, niwatake muendelee kutoa elimu na hamasa kwa watu wa maeneo ya mijini na vijijini,” amesema Msovela.

Amesema matumizi makubwa ya teknolojia hizo yanaweza kusaidia kuboresha ubora wa vyakula na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, huku uongezaji wa madini na vitamini ukiwa sehemu ya juhudi za kuboresha lishe na kukabiliana na udumavu kwa watoto mkoani Katavi.



